Ndoa yenye utata

1--------5 *SIMULIZI---NDOA YENYE UTATA....1.* *SEHEMU YA 1.* *UTANGULIZI* : Wahenga walisema, ukiona kwako kunafuka moshi ujue kwa mwenzio kunateketea. Ama kuna usemi mwingine usemao, kitanda usichokilalia huwezi kujua kunguni wake. Ndio, hayo ni maneno ya wahenga. Nami nasema hivi, usiitamani nyumba kwa uzuri wa bati lake kama haujawahi kuishi katika nyumba hiyo. Na jambo usilolijua ni sawa na usiku wa giza. Unajua ni kwa nini nimesema hivi? Simulizi tamu ya "NDOA YENYE UTATA" ndio itakuja kuthibitisha misemo hii yote. Ni simulizi tamu sana ambayo inasikitisha ndani yake. SONGA NAYO: "Ni muda mrefu sasa tunajuana, huu ni wakati sasa wa mimi na wewe kufunga ndoa yetu" "Ni kweli kabisa, unaonaje nikimaliza kabisa masomo yangu ili nipate degree yangu? "Hakuna tatizo mpenzi. Hilo nalo ni neno" "Basi sawa. Si unajua tena? Mambo mazuri hayataki haraka. Kuwa na subira mpenzi" Hayo yalikuwa ni mazungumzo kati ya kijana mmoja aitwaye Edo na msichana mmoja aitwaye Eliza. Hawa wote walikuwa ni wanafunzi wa chuo kikuu cha Dodoma (UDOM) Eliza na Edo walikuwa ni wapenzi wa muda mrefu hapo chuoni kwao, na huo ndio ulikuwa mwaka wao wa mwisho hapo chuoni. Baada ya kumaliza masomo yao, Edo alipata kazi katika kampuni moja maarufu sana hapa jijini Dar-es-salaam. Na Eliza alikuwa hajapata kazi. Hii haikufanya ndoa yao isifanyike kwani Edo hakutaka kabisa kupoteza muda katika hili. Edo alikwenda nyumbani kwa wazazi wa Eliza na kujitambulisha kwao. Wazazi hawakuwa na kipingamizi, baada ya kupata ujumbe huu wakamwita mtoto wao Eliza na kumwambia, "Kuna kijana anaitwa Edo, ametokea kukupenda na anataka kufunga ndoa na wewe" "Ninamfahamu vizuri sana kijana huyu. Niko tayari kuolewa na yeye kwa kuwa nampenda" Eliza alimwambia mama yake. "Unadhani huyu ni mtu sahihi kwako? Baba yake nae alimuuliza swali ili kutaka kujua" "Haswaa..! Sina mashaka nae kabisa" "Basi sawa. Mipango ya ndoa ifanyike ili muda si mrefu muwe mke na mume. Alimwambia" Edo alifurahi sana baada ya kusikia ombi lake la kutaka kumuoa Eliza limekubaliwa na wazazi wake. Bila kupoteza muda akapanga tarehe maalum ya kufunga ndoa yake. Edo aliwafahamisha ndugu na jamaa juu ya hili, ama kwa upande wa Eliza nae alifanya hivyo hivyo. Usiku wa deni hauchelewi kucha, mara ikafika tarehe ya kufunga ndoa yao. Ilikuwa ni ndoa ya fahari kubwa sana iliyohudhuriwa na watu wengi sana. Watu walikula, kunywa na kusaza. Kila aliyekuja katika harusi ile alifurahia sana. Mara ukafika wakati wa wazazi wa Eliza kumuaga binti yao mpendwa. "Hongera sana mwanangu, hakika hili ni jambo jema sana. Nenda katulie katika ndoa yako" Alisikika mama yake Eliza akisema. "Ndoa inahitaji uvumilivu. Unachotakiwa ni kuwa na subra. Ukizingatia haya utafanikiwa" Baba yake Eliza nae aliongeza neno. Haikuwa kwa wazazi wake tu, bali hata ndugu zake walimuasa juu ya hili. Ama kwa upande wa Edo nae wazazi wake walimuasa juu ya kumtunza mke wake na kumheshimu. Na sio mke tu, bali kuwaheshimu na kuwajali ndugu wa mke. Baada ya wazazi kumaliza kutoa wosia wao, hatimaye ndoa ikafungwa na Edo na Eliza kuwa kitu kimoja kama mke na mume. Safari ya Eliza kuelekea kwa mume wake ikaanza. Nderemo, vifijo na mayowe yalisikika kila mtaa. "Waliosema haolewi, mbona kaolewa" Hayo ni baadhi ya maneno yaliyokuwa yanasikika katika baadhi ya nyimbo zilizokuwa zinaimbwa na wapambe. Yaani ilikuwa ni siku ya furaha kubwa sana. Mara Edo na Eliza wakajikuta wako nyumbani kwao. Asikwambie mtu bwana, hakuna kitu cha fahari kama kufunga ndoa na mtu aliye katika ndoto yako. Na ndoa sio kitu cha masihara, watu wengi wanaitafuta nafasi hii adhimu. Ndio, kwani ndoa ni heshima na ndoa ni amani. Mtu aliye katika ndoa na bachela wana utofauti mkubwa sana. Watu walio katika ndoa wanalijua hilo. Mara ukafika usiku wa fungate, ni usiku wa kwanza wa Eliza na Edo kukutana wakiwa katika ndoa yao. Hakika, kila mmoja alikuwa na furaha na hamu na mwenzie. Bila kupoteza muda ukafika wakati wa tendo lenyewe, tendo hili ndilo linalokamilisha shughuli yenyewe. Huwezi kuwaita watu wanandoa pasina tendo hili kufanyika. Kila mmoja alihakikisha anamfanya mwenzie kuwa na furaha. Baada ya kumaliza kupeana haki zao za msingi, kila mmoja alikuwa amejipumzisha kitandani. Walikuwa wanasimuliana na kukumbushana baadhi ya mambo yao yaliyopita siku za nyuma. Na hii ni kawaida kwa wana ndoa. Wakiwa katika mazungumzo yao, Eliza akajikuta anaichukua simu ya mume wake Edo na kuanza kuperuzi. Ndio, hawa ni mwili mmoja sasa hivyo wanaweza kushirikiana katika baadhi ya vitu. Edo hakuwa na mashaka kabisa kwani muda huo alikuwa na furaha. Dakika mbili mbele, Eliza alionekana kutokuwa na furaha ghafla. Edo alijiuliza maswali, "Imekuwaje tena? Mbona Eliza amebadilika ghafla? Ni kitu gani kimetokea? Muda huo Edo alikuwa hajui kinachoendelea. Alishangaa sana baada ya kumuona mke wake Eliza akiwa anabubujikwa na machozi. "Ni kitu gani kinakuliza mke wangu? Eliza aliendelea tu kulia kwa uchungu. Edo alizidi kumhoji ili kutaka kujua. Ndipo Eliza alipomuonyesha ujumbe mfupi wa maneno (sms) alioukuta katika simu yake. Ulikuwa ni ujumbe wa kukatisha tamaa sana. Edo alishtuka sana baada ya kuuona ujumbe ule. Alijisikia vibaya sana. Alikosa amani. Je, ni ujumbe gani huo? Kumbuka hiyo ndio ilikuwa siku yao ya kwanza kabisa wakiwa katika ndoa yao. Unataka kujua kilichotokea? "Ndoa yenye utata" ndio jina la simulizi hii, mtunzi na mwandishi ni Saad Salum Mzola. Hakika hii ni zaidi ya simulizi, ungana na mimi katika sehemu ya pili ya simulizi hii. ********** USIKOSE ******** *SIMULIZI---NDOA YENYE UTATA....2.* *SEHEMU YA 2.* ILIPOISHIA: Edo alishtuka sana baada ya kuuona ujumbe ule. Alijisikia vibaya sana, alikosa amani. ENDELEA: Ujumbe ule ulikuwa umetumwa na Edina, inasemekana ni mchepuko wake wa siku nyingi sana. Mbaya zaidi ujumbe ule ulitumwa kama lisaa limoja hivi kabla ya Edo kufunga ndoa yake na Eliza. Inauma sana, na ujumbe wenyewe ulikuwa unasomeka hivi: "Hivi ni kweli Edo umeamua kuachana na mimi na kufunga ndoa na huyo mpenzi wako Eliza? Edo nae alimjibu Edina kwa kumwambia. "Ni kweli kabisa. Lakini nakuahidi, kuwa kwenye ndoa sio sababu ya wewe kulikosa penzi langu. Nitakuwa nakuibia kwa siri" "Nitafurahi sana kama utafanya hivyo" "Usijali kuhusu hilo Edina, nakupenda sana" Ni kama walikuwa wanachati muda mfupi kabla ya ndoa. Muda huo Eliza alikuwa hajui kabisa ni kitu gani kinaendelea? Hiki ndicho kitu kilichokuwa kinamliza Eliza kwani alikuwa anajua kabisa mbali ya Edo kuwa katika ndoa na yeye ataendelea kuwa na mahusiano ya kimapenzi na Edina. Hii ina maana Edo atakuwa msaliti katika ndoa yao. Asikwambie mtu bwana, Eliza alilia kupita maelezo. Siku ya furaha imekuwa ni siku ya huzuni kubwa sana kwake. Hivi inakuaje kitu kama hiki kinakutokea wewe? Haya mambo yasikie tu kwa mwenzio na wala usiombee yakukute. Edo akaanza kuchanganyikiwa. "Samahani sana mke wangu Eliza, najua umeumia sana. Naomba unisamehe kwa hili" "Hapana Edo, umeanza kunitisha siku ya kwanza tu ya ndoa yetu. Hakika nimeamini, kweli msaliti hana alama. Hivyo yaani" Edo alizidi kumbembeleza Eliza kwa kumuomba msamaha. Eliza alikuwa hamuelewi kabisa. Alipata mshituko mkubwa sana kutoka kwa mume wake Edo. Kuna msemo mmoja usemao, simu ya mpenzi wako ni sawa na kitunguu. Muda wowote inaweza kukutoa machozi. Na hiki ndicho kilichotokea kwa Eliza. Laiti kama asingefanya upekuzi katika simu ya mume wake Edo sidhani kama angeyajua haya. Kama ni sukari basi imeingia shubiri. Juhudi za Edo kumbembeleza Eliza huku akimuomba msamaha zilichukua muda mrefu sana bila mafanikio. Eliza alitamani ndoa yake isambaratike siku ile ile ya kwanza. Si unajua tena? Nyota njema huonekana asubuhi. Ni mapema sana ameujua udhaifu wa mume wake na ndio maana alikuwa na hofu. Edo alipiga magoti na kuzidi kumuomba msamaha mke wake Eliza ili amsamehe. Mwisho wa siku Eliza aliamua kumsamehe lakini kwa kishingo upande kwani mbali ya kumsamehe lakini alikuwa anaendelea na kilio. "Haya bwana, mimi nimekusamehe lakini sitakusahau. Sidhani kama kidonda kitapoa" "Usijali mke wangu Eliza, sitarudia tena" Eliza aliamua kuchukua shuka lake na kujifunika huku kilio kilichoambatana na kwikwi kikiendelea. Mara akajikuta anapitiwa na usingizi. Siku iliyofuata Eliza aliamka mapema sana, sidhani kama alipata usingizi wa ukweli kwani muda mwingi alikuwa na maluweluwe. Asubuhi ilipofika Eliza alionekana macho yake kuvimba sana kutokana na kilio cha usiku kucha. Muda huo Edo nae aliamka. "Habari ya asubuhi mke wangu, uko poa? "Niko poa tu. Umeamka salama? "Nimeamka salama, pole na uchovu" "Ahsante. Nae alimjibu" Eliza alionekana kuilazimisha furaha huku moyoni mwake akiwa na majonzi. Akiwa kama mama mwenye nyumba tena ni mke wa mwafulani, Eliza aliingia jikoni kwa ajili ya kumuandalia mume wake chai. Baada ya kumaliza kupika chai alimuandalia mume wake na kumuwekea mezani, kisha akamkaribisha. "Karibu chai mume wangu" "Ahsante sana mke wangu" Wakati Edo akiwa mezani tayari kwa kunywa chai Eliza alikuwa anaendelea na shughuli nyingine za pale nyumbani kwake. "Mke wangu...! Njoo tunywe chai kwanza" "Hapana mume wangu, sijisikii kabisa kula" "Kwa nini iwe hivyo mke wangu? Ina maana mambo ya jana bado unayo tu? Usifanye hivyo mke wangu. Nilishakuomba msamaha" "Nalijua hilo mume wangu. Nitakunywa chai baada ya kumalizika shughuli zangu" Edo alitumia nafasi ile katika kumbembeleza tena mke wake Eliza. Alifanya kila linalowezekana na kumshawishi mke wake. Hatimaye aliweza kumshawishi na Eliza alijumuika mezani pamoja na mume wake Edo katika kupata chakula cha asubuhi (Chai) Baada ya kumaliza kunywa chai, Edo na mke wake walifanya kazi za pale nyumbani kwa pamoja. Tena Edo aliamua kubaki nyumbani siku nzima ili kumfariji mke wake Eliza. Kwa kiasi fulani, Eliza alifarijika na kupunguza hasira. Mara wakajikuta wako katika mazungumzo ya kawaida kama ya mke na mume. Ilipofika jioni, walikula chakula cha usiku na kuanza kuangalia tv. Edo alihakikisha anafanya kila awezalo kuhakikisha anarudisha furaha ya mke wake Eliza. Aliweza kufanikiwa japo kwa asilimia kadhaa. Tangu siku ile Edo na Eliza walikuwa wanaishi maisha ya furaha na amani tele. Lakini Eliza alikuwa makini sana na mume wake kwani waswahili wanasema mtu aliyeumwa na nyoka hata kijani kikimgusa hushtuka. Hakutaka kumuamini moja kwa moja kwa kuwa tayari alishaujua udhaifu wake. Mjasiri haachi asili, Edo akajikuta anarudia tabia yake ya ajabu. Eliza aligundua kitu kutoka kwa Edo baada ya kumfanyia uchunguzi. Je, aligundua nini? Ni uamuzi gani alichukua safari hii? Majibu yake utayapata katika sehemu ya tatu. Simulizi inakwenda kwa jina la "NDOA YENYE UTATA" Ni bonge moja la simulizi. Kama kawaida, simulizi hii inaletwa kwenu na Saad Salum Mzoa. ********** USIKOSE ********** *SIMULIZI---NDOA YENYE UTATA....3.* *SEHEMU YA 3.* ILIPOISHIA: Mjasiri haachi asili, Edo akajikuta anarudia tabia yake ya ajabu. Eliza aligundua kitu kutoka kwa Edo baada ya kumfanyia uchunguzi. ENDELEA: Mara kwa mara Edo alikuwa anachelewa kurudi nyumbani, tena akirudi anakuwa amelewa chakari. Mke wake alipomhoji alimjibu hovyo. "Hivi mume wangu Edo, kwa nini siku hizi umebadili tabia? Kwa nini hauko kama zamani? "Haikuhusu..! Wewe ni mwanamke tu hapa nyumbani. Hutakiwi kunifuatilia mimi" "Kwa nini nisikufuatilie wakati ni mume wangu? Wewe na mimi ni mwili mmoja sasa. Kwani hujui? Achana na hiyo mifumo dume bwana" "Kwani humu ndani mwanaume ni nani? Yaani wewe ni kuku jike unataka uwike kama Jogoo? Eliza alikuwa anaumia sana, kwanza alikuwa na elimu ya kutosha. Lakini Edo alimzuia kujiendeleza kielimu zaidi na kumfanya mama wa nyumbani. Alikubaliana nae kwa kuwa ni mume wake. Lakini Edo aliitumia vibaya nafasi ile. Siku moja Eliza alishindwa kuvumilia. "Mume wangu Edo, ni bora nitafute kazi ili tusaidiane maisha hapa nyumbani? Eliza alimuomba mume wake Edo. "Ni nani alikwambia maisha yamenishinda hapa nyumbani mpaka wewe unisaidie? Edo alimjibu kwa dharau huku akimfokea. "Sina maana hiyo mume wangu. Tatizo pesa zako zote zinaishia kwenye kulewa tu" "Ni siku gani ulikosa kula hapa nyumbani? Wewe mwanamke sasa umeanza kunidharau" "Dharau ya nini mume wangu? Ina maana kukwambia hivyo ni dharau? Kwani una nini? "Sitaki ufanye kazi yoyote. Kitu ninachoweza kukusaidia ni kukufungulia salon ya kike" "Basi sawa..! Hata hiyo si haba mume wangu" Kwa shingo upande, Eliza alikubaliana na mume wake Edo. Kwa kiasi fulani aliweza kukidhi mahitaji yake binafsi. Eliza alivumilia kuishi kwenye ndoa yenye utata kama alivyoambiwa na wazazi wake kwamba ndoa ni uvumilivu. Kwa upande wa Edo yeye alizidi kuendelea na tabia zake za ajabu. Alifikia hatua ya kuwasiliana na wanawake zake wa nje mbele ya mke wake. Kweli wakati mwingine, ndoa ni ndoano. Wakati wengine wanafurahia maisha katika ndoa zao, wengine wanataabika na kujutia kwa nini waliingia kwenye ndoa? Mara kadhaa Eliza alikuta meseji za mapenzi kwenye simu ya mume wake Edo, kila alipomuonya Edo hakumsikiliza kabisa. "Hivi mume wangu, unayajua maumivu ya mapenzi? Ingekuaje mimi ningekuwa nakufanyia hivyo? Acha kuniumiza bwana" Ukweli ni kwamba, maumivu makali ya mapenzi yalikuwa ni sehemu ya maisha yake. Kuna wakati Eliza alishindwa kabisa kustahimili, alienda kwa wazazi wake na kuwaambia kila kitu kuhusu mume wake. Wazazi walimwambia kwamba aendelee kuvumilia kwani wanaume wote wako hivyo. Eliza hakuta kuamini maneno ya wazazi wake kwani aliona wanawake wengine wanaishi kwa amani katika ndoa zao. Kwa nini yeye iwe vile? Maisha ya ndoa yenye utata kwa Eliza yalimfanya avumilie mpaka wakapata watoto wawili. Eliza aliona kama amejitia kitanzini kwani alishindwa kudai talaka kwa kuhofia kuwapa taabu watoto wake. Hakutaka kabisa watoto wake walelewe na mama wa kambo. Kila kukicha afadhali ya jana, mwisho wa siku Eliza alikaa na mume wake na kumwambia. "Kwa sasa uzalendo umenishinda, ni bora unipe talaka nikaanze maisha mapya kabisa" "Unasemaje wewe? Mimi najua kuoa tu. Na wala sijui kuacha. Huo ndio utaratibu wangu? "Kama ni hivyo, basi badili tabia zako mume wangu. Upendo wa wanandoa uko wapi? Ni kama alikuwa anampigia mbuzi gitaa. "Kwani mume wangu ananichuliaje? Yaani haya ndiyo malipo ya kumpenda kwa dhati? Kwani nina kasoro gani? Uvumilivu unanishinda" Eliza alikuwa ni mtu wa kulalamika muda wote wa maisha yake. Alikuwa hana furaha kabisa. Siku moja Eliza alikutana na kijana mmoja aitwaye Daniel, hii ilitokea maeneo ya Gongolamboto. Ndio, ni kituo cha mabasi ya kwenda nyumbani kwao Majohe. Kijana huyu walikuwa wanajuana siku nyingi sana. Kabla ya Eliza kuwa na mahusiano ya kimapenzi na Edo aliwahi kuwa na uhusiano na kijana mmoja aitwaye Jamali. Kipindi hiko alikuwa ni mwanafunzi wa sekondari. Mahusiano ya Jamali na Eliza yalivunjika baada ya Eliza kwenda kujiunga na chuo kikuu cha Dodoma (UDOM) Huko ndiko alipokutana na Edo na kuwa mtu wake wa karibu. Mwisho wa siku wakawa wapenzi wakubwa sana. Kama ulikuwa hujui, Jamali na Daniel walikuwa marafiki wakubwa sana. Isitoshe walikuwa wana undugu wa kiaina. Kaka yake Daniel alimuoa dada yake Jamali. Na Daniel alikuwa anaujua uhusiano wa kimapenzi uliokuwepo kati ya Jamali na Eliza kwa kipindi hiko. Hata Eliza alipoachana na Jamali, Daniel aliumia sana. Jamali alimueleza Daniel ni jinsi gani alivyokuwa anampenda Eliza? Kuna wakati, Daniel aliwahi kuwasuluhisha Jamali na Eliza ili waendelee kuwa na mahusiano. Lakini Eliza hakuwa tayari kwa kuwa alimuona Jamali si mtu wa hadhi yake. Jamali aliumia sana lakini akaamua kukubali matokeo kwa kuwa anajua kabisa mapenzi hayalazimishwi. Ni mikaka mingi sasa, Jamali hayuko duniani. Kuna wakati aliugua ghafla na kufariki. Kitendo cha Danieli kukutana na Eliza maeneo ya Gongolamboto kikawafanya wakumbuke mambo mengi sana ya siku za nyuma. Daniel yeye alikuwa anaishi maeneo ya Mvuti, ni nje kidogo ya jiji la Dar-es-salaam. Nae kituo chake cha mabasi ya kwenda kwao ni Gongolamboto. "Habari yako Eliza, uko poa? Daniel alimsalimia. "Niko poa tu Daniel, za siku nyingi" "Njema tu shemeji yangu. Umepotea sana. Kwani unaishi wapi siku hizi? Alimuuliza" "Kwa sasa naishi Majohe, wewe unaishi wapi? "Mimi naishi Mvuti. Karibu sana nyumbani" "Ahsante sana, vipi familia yako? Muda huo Eliza alikuwa anajua kabisa kama Daniel ana mke na watoto wawili. "Namshukuru Mungu. Sijui wewe? "Hata mimi namshukuru Mungu pia" "Unaonaje tukibadilishana namba za simu? Daniel alimwambia shemeji yake wa zamani. "Sio mbaya...! Eliza akamtajia namba zake" Daniel nae alifanya hivyo kisha wakaagana. Tangu siku hiyo Daniel alikuwa anawasiliana na Eliza mara kwa mara. Siku moja Daniel alimpigia simu Eliza na kumtaka wakutane maeneo ya Gongolamboto. Alimwambia kwamba alikuwa na mazungumzo na yeye. Eliza hakukataa wito, akaamua kukutana nae. Je, ni mazungumzo gani hayo? Sehemu ya nne itakuwa na majibu yote. Simulizi inakwenda kwa jina la "NDOA YENYE UTATA" Mtunzi na mwandishi wa simulizi hii ni Saad Salum Mzola. Ni simulizi tamu sana yenye uhalisia na maisha ya kweli. ********** USIKOSE ********** *SIMULIZI---NDOA YENYE UTATA....4.* *SEHEMU YA 4.* ILIPOISHIA: Eliza hakukataa wito, akaamua kukutanae nae. ENDELEA: Kama kawaida, walikutana katika bar moja maarufu sana pale Nyama choma jirani sana na Maliasili. Kisha wakaanza mazungumzo. "Niambie Eliza, ni siku nyingi sana tumepoteana. Umeamua kutupa jongoo na mti wake. Usifanye hivyo shemeji yangu" "Hapana shemeji, ni majukumu ya kimaisha. Si unajua tena usawa tuliokuwa nao kwa sasa? "Ni kweli kabisa Eliza, hali ya maisha imekuwa ngumu sana. Kila kukicha afadhali ya jana" "Umeona eenh shemeji yangu, we acha tu" "Ndio hivyo tena, nikuulize swali shemeji? "Niulize tu Daniel. Uko huru kwa hili? Eliza alimpa nafasi Daniel ya kumuuliza. "Uko sawa kweli shemeji? Mbona unaonekana kama una mambo mengi sana kichwani? Eliza alinyamaza kwa sekunde kadhaa. Kisha akamwambia Danieli kwamba. "Niko sawa shemeji yangu. Kwani umegundua kitu gani kutoka kwangu? Niambie shemeji" "Eliza ninaemjua mimi sio wewe. Kwanza umepungua sana, halafu unaonekana una mawazo mengi sana. Tatizo ni nini? "Mbona niko sawa tu? Sina tatizo lolote" "Haya bwana, siku zote mficha maradhi mauti humuumbua. Endelea tu kunificha hivyo hivyo" Eliza aliinamisha kichwa chake chini, mara machozi yakaanza kumtoka kwa uchungu. "Ni kitu gani kinakuliza Eliza? Hebu niambie" Eliza baada ya kuona kwamba Daniel amegundua kitu kutoka kwake akamwambia. "Daaaah..! Sioni sababu ya kukuficha shemeji yangu. Niko katika wakati mgumu sana" "Ni kitu gani kinakusibu? Naomba usinifiche" Eliza aliamua kumsimulia Daniel mkasa mzima kuanzia mwanzo mpaka mwisho. Hakutaka kumficha chochote kile. Daniel aliposikia vile, akaamua kuchukua kinywaji chake na kupiga fundo mbili za haraka haraka. Kisha akasema, "Pole sana shemeji yangu. Nakuonea huruma sana. Wewe sio mtu wa kufanyiwa hayo. Hivi wanaume wengine wanajitambua kweli? "Kwa nini unasema hivyo shemeji yangu? "Acha nikwambie ukweli Eliza, watu wanaumia sana juu yako. Nashangaa yeye anakutesa" "Jamani shemeji..! Acha masikhara yako bwana. Ni akina nani hao? Mtu mwenyewe sina hata maajabu. Tazama nilivyokondeana" "Huwezi amini shemeji yangu. Mimi mwenyewe ni mmoja wa watu hao? "Ahahaha..! Ujue Daniel una vituko sana. Hivi hujaacha tu makuzi yako? Una balaa wewe? "Hapana Eliza, kwa kweli nilikuwa naumia tangu siku nyingi sana. Leo nimeamua kukwambia ukweli. Niko serious kabisa" "Mmmmh..! Yamekuwa hayo tena? Kwani hujui kama mimi ni shemeji yako? Acha vituko" "Nalijua hilo shemeji. Sheria zimewekwa ili zivunjwe. Kwanza niliumia sana ulipoachana na rafiki yangu na kumkabidhi penzi huyo boya" "Aaah..! Usimwite mume wangu boya bwana" "Hana lolote, ni mshenzi sana. Yaani natamani nilipe kisasi. Ningefurahi kama ungenipa nafasi. Jamali aliumia sana kukupoteza" Eliza aliposikia habari za Jamali aliumia sana. Ghafla akaanza kuulia kwa uchungu. "Pole sana Eliza, huu ni wakati sasa wa mimi kukufuta machozi. Hebu nipe hiyo nafasi" "Hapana Daniel, siko tayari kwa hilo. Tuendelee kuheshimiana kama mtu na shemeji yake. Nilikuwa nampenda sana Jamali" "Kama ni hivyo, mbona uliamua kumuacha na kuwa nae huyo mdwanzi? Tazama anavyokutesa. Amekuwa mtu mbaya sana" "Ndio hivyo tena, majuto ni mjukuu. Haya yameshatokea. Unadhani nitafanya nini? Eti Eliza alimkumbuka sana Jamali. "Tuachane na hayo Eliza. Kwa sasa mimi ndiye nitakuwa mrithi wa rafiki yangu Jamali" "Hapana shemeji. Hii haitawezekana" "Okay, sio kesi. Kama hauko tayari Mimi sikulazimishi. Lakini elewa nakupenda sana" "Jamani Daniel, lakini wewe si una mke? "Mbona mume wako ana mke lakini anakufanyia mambo kama hayo? Eliza alikaa kimya kwa muda, alikuwa anawaza mambo mengi sana. Hakuwa tayari kumsaliti mume wake Edo kwani alikuwa anampenda sana. Aliona ni dhambi kubwa kufanya vile. Ukimya ulitawala pale mezani, muda huo Daniel alikuwa anachezea tu simu yake. Baada ya ukimya wa muda mrefu, Daniel alimuuliza. "Eeenh..! Bila shaka ulikuwa unanifikiria mimi. Je, uko tayari kuwa na mimi? Nakupenda sana" "Hapana Daniel..! Samahani sana, siko tayari kwa hili. Pia naomba nisamehee kama nimekukwaza. Sitaki unichukie kwa hili" "Hakuna tatizo Eliza. Siwezi kukulazimishi katika hili. Na wala sina kinyongo na wewe" Baada ya kumaliza vinywaji vyao wakaagana na kila mmoja kurudi nyumbani kwake. Wakiwa njiani kila mmoja alikuwa anamuwaza mwenzie. Yaani walikuwa katika wakati mgumu sana. Kwa upande wa Daniel ilikuwa hivi: "Bado sijakata tamaa, ni kawaida ya wanawake kuwa wagumu sana kwa mara ya kwanza kukubali ombi la wanaume la kimapenzi" Huko upande wa pili nako, Eliza aliwaza: "Hivi ni kweli Daniel yuko serious na hili? Ina maana hajui kama mimi ni shemeji yake? "Sijui nimkubalie? Halafu itakuwaje sasa? Yaani Eliza alikuwa katika sintofahamu kubwa. Baada ya kufika nyumbani akaendelea na shughuli zake za kawaida. Muda wote Daniel alikuwa anamjia kichwani mwake. Mara mume wake Edo akarudi kutoka kazini, kama kawaida yake alikuwa yuko chakari kwa ulevi. Eliza alimtazama kwa kina kisha akajisemea mwenyewe moyoni mwake: "Laiti kama ungejua kuna watu wanaitafuta nafasi hii adhimu, usingenifanyia vibweka" Eliza aliendelea kuishi na mume wake Edo maisha ya utata siku zote katika ndoa yake. Siku moja Eliza alikata shauri: "Nahisi uzalendo unanishinda, huu ni wakati sasa wa mimi kupata mtu wa kuniliwaza. Bila shaka Daniel atakuwa mtu sahihi kabisa" Kipindi hiko Daniel alikuwa amepoteza mawasiliano na Eliza kwa siku kadhaa. Eliza aliamua kumtumia ujumbe mfupi: "Niambie shemeji yangu. Naona umenisusa" Daniel alipouona ujumbe ule alimjibu. "Hapana Eliza, ni mambo fulani tu. Lakini nakukumbuka sana. Mimi na wewe tena? "Eti eeenh? Nilijua umesusa baada ya mimi kukukatalia ombi lako la kutaka kuwa na mimi" "Hapana..! Huwezi kumlazimisha Ng'ombe kunywa maji. Hilo ni jukumu lake mwenyewe" "Daaah..! Nimemiss sana vituko vyako" "Eti eeenh? Kama vipi tupange siku tukutane mahali pale pale ili tubadilishane mawazo" "Basi sawa. Nikipata nafasi nitakufahamisha" Siku moja Eliza alichukua simu yake ya mkononi na kumpigia Daniel. Alimwambia hivi: "Kama utakuwa na nafasi siku ya kesho naomba tukutane mahali ili tuyajenge" "Hakuna tatizo, nina muda wa kutosha tu" Siku iliyofuata Eliza na Daniel walikutana mahali kwa ajili ya mazungumzo yao. Je, ni mazungumzo gani hayo? Mimi na wewe hatujui. Ungana na mimi katika sehemu ya tano ya simulizi hii tamu sana. Simulizi inakwenda kwa jina la "NDOA YENYE UTATA" Ni bonge moja la simulizi, hii si ya kuikosa. ********** USIKOSE ********** *SIMULIZI---NDOA YENYE UTATA....5.* *SEHEMU YA 5.* ILIPOISHIA: Siku iliyofuata Eliza na Daniel walikutana mahali kwa ajili ya mazungumzo yao. ENDELEA: Kama kawaida yao, walikutana katika bar ile ile waliyokutana kwa mara ya kwanza. Bila kupoteza muda mhudumu wa ile bar akaja na kuanza kuwahudumia. Baada ya kuagiza vinywaji wakaanza mazungumzo yao. "Niambie Eliza, hivi kwa nini umekuwa mgumu sana katika kutoa maamuzi? Ni kitu gani kinakufanya ufikirie kwa muda mrefu? Daniel alimuuliza swali Eliza. "Unajua nini Daniel, ninatakiwa nitumie muda mwingi sana kwa ajili ya kumchunguza mtu ili yasije kunikuta kama haya yanayonisumbua" Eliza nae alimjibu Daniel. "Una maana gani kusema hivyo? "Ni swali zuri sana. Nilifanya makosa makubwa sana katika kuchagua. Hebu tazama Edo anavyonifanyia kwa sasa. Sitaki kurudia makosa kama niliyofanya mara ya kwanza? "Kwa hiyo una mashaka na mimi? "Hapana, nimeamua nichukue tahadhari kwa kuwa siku zote msaliti hana alama. Hata Edo alikuwa na muonekano kama huo huo wako" "Sikiliza Eliza, unafanya makosa makubwa sana ya kunifananisha mimi na Edo" "Ndio hivyo Daniel..! Wanaume mmekuwa makatili sana katika mapenzi. Sijui kwa nini? "Naomba uniamini Eliza. Nakupenda sana. Sitakaa kukuumiza kwa kuwa najua historia ya mapenzi yako. Unahitaji faraja kwa sasa" Daniel alijitahidi kwa kiasi kikubwa sana kumuaminisha Eliza kwamba yeye ni mtu sahihi kwake hivyo asiwe na wasi wasi kabisa. Naam, jamaa alikuwa anajipasia mwenyewe. Si unajua tena wanaume wanapohitaji penzi kutoka kwa mtoto wa kike? Mara Eliza akajikuta anamkubalia. Hakuwa na kipingamizi tena. Bila kupoteza muda wakamwita mhudumu wa ile bar ili awape utaratibu mzima wa pale. "Samahani sana, tunaweza kupata chumba kwa ajili ya kupumzika? Daniel alimuuliza" "Yeah..! Huduma hiyo inapatikana pia" "Basi sawa. Hebu tufanyie utaratibu huo" Bila kupoteza muda mhudumu akawaandalia chumba kizuri sana. Daniel akafanya malipo kisha wote wawili wakaingia chumbani. Mapenzi ni kitu cha ajabu sana, Daniel na Eliza walikuwa ni mtu na shemeji yake lakini muda mfupi baadaye wameenda kuwa wapenzi. Kifuatacho I.T.V, ni mwendo wa kupeana tu mapenzi moto moto. Kumbuka hao wote wawili wako katika ndoa zao, mara wakajikuta wanafanya usaliti bila ya wenzi wao kujua. Ndoa ni mchezo wa bahati nasibu, kuwa makini sana kabla hujaamua kuucheza. Na unapoingia katika ndoa usiingie na matokeo kwani mchezo huu una matokeo ya kikatili sana. Sikwambii wewe unayetaka kuoa au sikutishi ili uogope, bali nakupa tahadhari. Eliza na Daniel waliivunja ile amri ya sita kama hawana akili nzuri vile. Baada ya kumalizia kufanya ufuska wao wakaagana na kila mmoja kurudi nyumbani kwake. Tangu siku hiyo Daniel na Eliza wakawa wapenzi. Eliza alifanya kwa tahadhari kubwa sana ili mume wake Edo asijue, na Daniel nae ilikuwa hivyo hivyo. Hii ilikuwa ni tofauti kabisa na Edo kwani yeye alikuwa hana tahadhari wala kificho kiasi cha Eliza kugundua udhaifu wake mapema sana. Eliza alijua kabisa usaliti ni mbaya. Tena alikuwa anajua kabisa mapenzi yanauma sana kuliko hata kidonda. Na ndio maana hakutaka kabisa kumuuza Edo kama alivyokuwa anafanyiwa yeye. Daniel na Eliza walikuwa wanakutana kila wakati kufanya mapenzi. Ndani ya muda mfupi, Eliza akajikuta ni mtu mwenye faraja. Yale maumivu ya kusalitiwa na mume wake Edo yakaanza kupungua. Kufanya malipizi katika usaliti sio dawa bali hupunguza maumivu. Ndoa ndoano, Eliza na mume wake Edo wakawa katika mapenzi ya usaliti. Daniel nae alikuwa anamfanyia usaliti mke wake bila ya huruma yoyote. Huwezi amini, mke wa Daniel alikuwa hajui kabisa kinachoendelea. Ukisikia ndoa yenye utata ndio hii. Siku hizi wanandoa wamekosa uaminifu kabisa. Usiposalitiwa asubuhi basi utasalitiwa jioni. Mambo yanakwenda vululu vululu. Mapenzi aliyokuwa anayapata Eliza kutoka kwa Daniel yalimfanya awe na mabadiliko makubwa sana pale nyumbani kitu kilichomfanya Edo ajiulize maswali. Hapo awali, Eliza alikuwa ni mtu wa kulalamika sana pindi Edo anapochelewa kurudi kazini lakini hakuwa hivyo tena baada kuwa katika mahusiano na Daniel. Edo alirudi nyumbani usiku wa manane, wakati mwingine alikuwa harudi kabisa nyumbani. Lakini Eliza alikuwa kimya kabisa. Hakuonyesha kukerwa na tabia ile. "Mbona siku hizi Eliza hayuko kama zamani? Ina maana siku hizi hana wivu na mimi? Edo alijiuliza maswali mwenyewe bila kupata majibu. Alishindwa kumuelewa kabisa. "Haiwezekani, sio bure. Lazima nimfanyie uchunguzi. Nahisi kuna kitu kinaendelea" Siku moja wakati wa mchana, Eliza alimuomba Daniel amtumie hela ya vocha ili waweze kuwasiliana. Bila kupoteza muda Daniel alimtumia shilingi elfu kumi. Kwa bahati mbaya siku ile Edo alikuwa nyumbani. Alisikia sauti ya ujumbe mfupi ukiingia katika siku ya Eliza. Akaanza kuhisi jambo. Edo alikuwa na wivu sana japokuwa yeye ndiye aliyekuwa msaliti mkubwa katika ndoa yao. Edo alikuwa anaivizia simu ya Eliza bila ya yeye mwenyewe kujua. Wakati anafanya hivyo, Eliza alikuwa hajui kwamba Daniel amemtumia kiasi kile cha pesa kwani alimuomba wakati wa mchana. Eliza alikuwa anaendelea na mapishi ya chakula cha jioni huko jikoni, mara akajikuta ameisahau simu yake chumbani. Edo aliitumia nafasi ile kufanya upekuzi katika siku ya mke wake. Ndipo alipokutana na ujumbe usemao. Umepokea kiasi cha shilingi elfu kumi kutoka kwa Daniel Ngwasi. Salio lako kwa sasa ni shilingi elfu kumi na tano. Daniel alijiuliza, "Ni nani huyu aliyemtumia pesa mke wangu? Na kwa nini afanye hivi? Haiwezekani" Edo aliichukua namba ile na kuisevu katika simu yake. Kisha akamwita mke wake Eliza. "Kuna ujumbe mfupi umeingia katika simu yako. Kuna pesa umetumiwa na Daniel. Unaweza kuniambia huyo Daniel ni nani wako? Eliza alishtuka sana baada ya kusikia vile. Alikuwa na hofu kubwa sana, midomo yake ikaanza kutetemeka kwa woga utadhani alikuwa amekula makaa ya moto. Unajua ni kitu gani kilitokea? Utamu wa simulizi hii unaanzia hapa. Kweli nimeamini, mtenda akitendewa huisi ameonewa. Simulizi inakwenda kwa jina la "NDOA YENYE UTATA" ********** USIKOSE ********** Full 1000

Post a Comment

TOA MAONI YAKO HAPA

Mpya zaidi Nzee zaidi

Ads related

Smartwatchs