My heart beat

1 - 22 MY HEART BEAT:01 Jina langu naitwa HOPE, jina ambalo naweza kusema linaendena na mimi karibia kila kitu, jina ambalo linafanya nishindwe hata kulala usingizi bila kufikiria nyumba yangu, namaanisha familia yangu. Familia yangu ambayo ni mama na mdogo wangu wa kiume ambayp wote wanaishi kwa kunitegemea mimo. Sijawahi kujisikia vibaya kuwa kinara wa familia yangu. Hii huwa inanipa Nguvu, hii huwa inanijenga, hii huwa inanipa tumaini la kuinuka tena, kuona mbele na kupambana na maisha kwa nguvu sana, kwasababu ninajua ninao watu nyuma yangu ambao hawali bila mimi kuamka, hawaendi shule bila mimi kupambana, hakuna kwenda hospitali, kununua dawa wala chochote bila tumaini lao kufanya kazi, hii inanifanya nijione ninatumia vizuri nguvu zangu na uwepo wangu duniani. Kitu kizuri ni kuwa, mbali na haya yote, tangu baba kufariki, mama yetu alitulea vizuri, alituweka karibu na Mungu, tunampenda Mungu, tunamuamini Mungu ndiyo maana pamoja na yote haya bado tunapambana sana kuhakikisha kila kitu kinakuwa sawa hatukati tamaa. Unaweza ukawa unajiuliza, kwanini mimi ndiyo nifanye majukumu yote haya na mama yangu yupo?. Ni kweli, lakini mama yangu kwa muda hana uwezo wowote ule, anaumwa sana, ni mtu wa kitandani, hawezi kufanya lolote zaidi ya kuzungumza tu. Amepooza, hana nguvu tena, wanao uguza wananielewa, ni mama yangu huyu, ni kila kitu kwangu, unajua namna inaumiza kumuona nguzo ya familia, mama ambaye mlitakiwa kuwa mnasaidiana hapa na pale, hili na lile hawezi tena amelala tu kitandani. Siwezi kusema mara ngapi nimelia na Mungu, nimelia peke yangu, nimeumia kumshuhudia mama yangu akifanya kila kitu, kila kitu kitandani. Inauma sana, nitafanya nini na mimi ndiyo dada mkubwa mdogo wangu bado mdogo na anatakiwa kusoma. Sijataka kumuacha awe kijana wa mtaani na mimi nipo. Ndiyo maana niliamua kubeba jukumu kuhakikisha kidogo chetu, kinafaa kwenye maisha yetu.
MY HEART BEAT:02 Kwa mazingira haya sitaki hata kuelezea kwetu panavyo fanana, utakuwa umepata picha kamili, basi haya ndiyo maisha yangu na mama yangu na mdogo wangu. Nilikuwa nina kazi nyingi sana mwanzo na maanisha mimi sichagui kazi. Yoyote kwangu twende, kufua, kufanya usafi, kukaa na mtoto, yoyote tu ili mradi kazi. Kwa wakati huu sasa, nilikuwa nimepata meza sokoni ingawa sio yangu kabisa, ni kama nimejiegesha tu mwenye meza akihitaji ataendelea na meza yake na mimi nitaendelea na mishe zangu. Ndiyo maisha yetu haya kubebana tukikwama hata kama kuna gharama unatakiwa kulipa. Nakumbuka sana siku hii, nilichelewa kiasi kuamka. Na nilipo amka niliingia chumbani kwa mama moja kwa moja. Mama yangu aliponiona alitabasamu, nilitabasamu pia nikisema “Mama Hope, shikamoo.” Mama alitabasamu tena akisema “umechelewa kuamka leo mama wa mimi, upo salama kweli?” Nikatabasamu huku nikijinyoosha nyoosha na kumjibu “mama yangu mzuri, nipo salama. Vipi wewe upo salama?” Mama alinitazama, akajitazama na kunijibu “nipo salama binti yangu, namshukuru Mungu.” Nikamuuliza mama “vipi kaka mkuu?.” Mama alinitazama na kusema “ameenda shule.” Nikashangaa na kusema “makubwa, hajaniamsha kutaka pesa leo, sio kawaida ujue.” Mama alicheka akisema “ukiona hivyo ujue kakua kaka yako.” Nikacheka nikisema “usinichekeshe mama, wakukua atakuwa yule.” Mama alitabasamu tu.
Basi nilitoka na baada ya muda nilirudi na ndoo ya maji, nilianza kumuhudumia mama yangu kwanza pale kitandani. Nilihakikisha mama yangu anakuwa safi kabisa. Mama alinitazama na kusema “Pole mwanangu, na asante kwa kunilea.” Nilitabasamu na kisha nikamwambia “wewe ni mama yangu, nina amini tu mama ipo siku isiyo na jina, utaamka kwenye hiki kitanda na wewe utatulea mimi na kala yangu si ndiyo mama.” MY HEART BEAT:03 Mama kama vile alitaka kulia, nilimtazama na kuona hilo. Nikamzuga pale kwa kuinuka na kwenda zangi nje. Kisha nikaandaa chakula chake harakaharaka na niliporudi mama alinitazama akaniuliza “sasa mwanangu si utachelewa kwenye kazi zako.” Nilitabasamu nikisema “sio mbaya ikiwa wewe ndiyo sababu nimechelewa. Najua maombi ya mama yangu mbele ya Mungu juu yangu yalivyo na kibali.” Mama alitabasamu, nikasogea na kuanza kumlisha chakula. Nilihakikisha mama yangu ana shiba ndiyo sasa na mimi najiandaa kwaajili ya kwenda sokoni.Mama akiwa peke yake nyumbani na sina namna. Niseme nini tena juu ya sokoni namna kunachangamka. Nilipofika wenzangu tayari walikuwa wameanza kazi. Na mimi nikaanza kupanga vitu kwenye meza yangu, sikioni nasikiliza zangu mziki. Nilikuwa na vitu vizuri sana siku hii lakini kitu cha ajabu, sio nyanya wala kituu, sio karoti wala oho, sio chochote kwangu kinauliziwa hata bei yake wakati vitu ni vizuri sana hata mimi naona kabisa ni vizuri. Mpaka mida ya saa nane, sina hata la maana nililofanya wakati naona wenzangu wanauza roho inaniuma sana, mimi nipo nimetingwa na kusinzia na kufukuza nzi tu. Niliona isiwe shida, kama kazi hii haijanilipa leo bora nikamlishe mama yangu mchana. Nilimuaga jirani yangu nikiwa na maumivu tu nawaza familia yangu itaishi vipi leo kama mambo yenyewe ndiyo haya. Mama yangu eenh, dawa zake tutanunua vipi kama haya ndiyo mambo yenyewe. Kila nikiwaza ninapata mawazo. Nilifika nyumbani, mama yangu alikuwa tu kitandani. Yupo machp ila hana cha kufanya. Namuhurumia tu. Nilipofika mlangoni kwake nilisimama kwa muda machozi yakinitoka huku nami nikiyafuta. Mara mama yangu aliita “Hope mwanangu!!!” Haraka nikajiweka sawa na kuitikia “abee mama!” Mama akaniuliza “mbona unasimama tu mlangoni na husemi umefuata nini?” Nikasema tu “mama nimeona nije kukupatia chakula mwenyewe.” Mama alisema “binti yangu unapenda kuteseka. Kaka yako akitoka shule tu anakuja kunilisha.kazi sasa umemuachia nani?” Nilinyamaza kwa muda na baada ya hapo sasa, nilitoka na kufuata chakula kisha nikarudi na kukaa kando ya mama na kuanza kumlisha. MY HEART BEAT:04 Nilianza kumlisha mama kijiko cha kwanza, cha pili , tatu na nne. Mama yangu alinidaka mkono. Nilimtazama, mama yangu aliniambia “wewe ni binti yangu, ninakufahamu vizuri Hope. Ndiyo sina uwezo wa kuamka hapa, ila uwezo wangu kama mama upo palepale niambie, una shida gani?” Nilimtazama mama yangu, nilijikuta ninashindwa kujizuia kulia. Nikaweka sahani chini na kumkumbatia mama yangu nikisema “mama tumemkosea nini Mungu lakini mama, mbona maisha yanakuwa magumu namna hii, tumekosea nini?, mbona tunapitia yote haya?” Mama alinibembeleza na kisha akaniuliza “nini kimetokea mwanangu?” Nilimtazama mama na kusema kwa upole “mama, tangu niende sokoni, sijauza chochote cha maana mama zaidi ya hii elfu mbili. Wenzangu wanauza mimi nasinzia tu, sasa ndiyo nini na vitu vizuri ninavyo. Ni maisha gani haya mama, vikiharibika itakuaje sasa.” Mama alinitazama usoni, na kisha alisema “Hope binti yangu, acha kulia.” Nilimtazama mama yangu, kisha alitabasamu na kusema “sali. Sali binti yangu, ombea biashara yako. Maombi ndiyo ufunguo pekee ambao unafungua vitu haviwezi kufunguka kwa ufunguo wowote ule. Sali, usichoke kusali ukiwa kwenye maumivu ya namna yoyote ile. Kuna namna maombi yanafariji tofauti na mimi, au yeyote katika dunia hii anaweza kukufaraji. Maombi peke yake ndiyo yanaweza kukuletea majibu ya maswali yako yote. Kila kitu kipo kwenye hayo maombi. Usisali tu kwasababu unatakiwa kusali, sali kwa ushahidi, sali ukimaanisha, sali kwa uhakika na unataka kwelikweli kusali. Wengi sana huenda mbele za Mungu kwasababu wanataka tu kwenda ila hawana nia ndani yao, hawajui wamuamini au wasimuamini. Muhimu kuliko hata haya maneno yangu kwenye yote hayo unayolalamika hapa Sali.” MY HEART BEAT:05 Nilimtazama mama na kuvuta pumzi yangu, nilitaka kulalamika tena na mama yangu alitabasamu akisema “acha, acha kulalamika binti yangu. Mshukuru Mungu hata ukipata kidogo, mshukuru Mungu kwa kila namna. Unajua mwanangu biashara haitaki mashindano, kwasababu kila mtu na bahati yake, biashara haitaki haraka, kila mtu na mwendo wake, na biashara haitaki mashindano kila mmoja na siri yake. Umechagua kusali basi sali hata kama sio kikubwaaaaaaaa, lakini umepambania haki yako.” Nilishika mikono ya mama yangu na kumtazama nikisema “asante sana mama, nakuahidi nitapambana zaidi.” Mama alitabasamu na kusema “unapo pambana usisahau Sali.” Nikacheka na kuchukua sahani yangu nikisema “ndiyo maana nakupenda.” Wakati nasema hivyo mdogo wangu alikuwa anaingia akisema “mnapendana wenyewe kama kawaida yenu.” Tukacheka nikisema “cha wivu kafika sasa.” Tukacheka na mdogo wangu alisema “daaah!!, ungejua nilivyo kuwa nakimbia nimuwahi mama, kumbe ningetembea zangu tu.” Tukacheka tena huku nikisema “hata hivyo hujachelewa kaka wa mimi, njoo hapa uendelee mimi nikaendelee na kazi. Si unajua lakini kazi zako?” Mdogo wangu alisema kwa kunitazama “usijali kabisa dada, muda ukifika kila kitu nitaweka sawa. Niambie sasa nitoe kitu leo au utakuja mwenyewe.” Nilijikuta nacheka nikisema “weeee, sitaki mapishi yako tena. Jana kidogo tuhare kisa pishi lako. Nitakuja nipike mwenyewe.” Mama alicheka sana, huku mdogo wangu akisema “mama si unaona mwanao, ina maana mpaka muda huu hajalikubali sotojo langu.” Tukacheka sana, tulijikuta tunacheka. Baada ya haya mazungumzo, niliingia chumbani kwangu. Nilipofika tu nilipiga magoti katikati ya chumba changu nikiwa nataka kwelikweli kubariki kazi za mikono yangu, kuziombea kibali zipate kuonekana machoni pa watu, kufanya zivutie kwa watu. Kwasababu Mungu anajua umuhimu wa biashara yangu katika familia yangu. Baada ya hapo niliaga nikisema “ndugu zangu baadaye.” Nilisikia mdogo wangu akisema “kazi njema dada, ukipata pesa leo usisahau nyama.” Nikacheka na mama nilisikia akicheka huku nikisema “mjinga sana wewe.” MY HEART BEAT:06 Nilianza kutembea kurudi kwenye mihangaiko yangu. Sio kama Soko ni karibu sana. Ni parefu kiasi unaweza kupanda gari lakini mimi tena nimeamua zangu tembea. Nikatembea mpaka kufika pale nimechoka. Niliweka meza yangu sawa kisha niliketi. Niliketi kwa muda kama nusu saa hivi ilikuwa imepita. Nikiwa nimejiinamia nikasikia sauti “binti hujambo?” Haraka niliinua kichwa changu, kisha tabasamu la biashara likaja usoni, alikuwa ni baba mtu mzima, na kijana smart mbele yangu. Nilisalimia nikiongezea maneno ya biashara “karibuni sana, karibuni sana.” Huyu baba alinitazama akisema “nashukuru sana.” Kisha nikamtazama huyu kaka, yeye anazungumza huku anatabasamu akisema “unauzaje hivi, hapa, vipi pale, naomba na pale.” Unajua ni kama ndoto, vile anataka nyanya sado, vitunguu sado, karoti, oho, matunda na mbogamboga kama nisimame nimkumbatie mteja ila siwezi.” Nilifuata mfuko haraka haraka na kuanza kuwahudumia kama ndoto vile, nawahudumia huku natabasamu, mara huyu kaka nikigusa nyanya na yeye kwa bahati mbaya ananigusa hapo akiwa ananionesha nina mtazama natabasamu tu. Unajua mpaka siamini kama nimeuza mimi, siamini kabisa hawajaenda genge lingine zaidi ya genge langu. Walipomaliza mzeee akauliza “unatudai bei gani?” Nikataja huku natabasamu. Huyu kijana akawa anatoa pesa huku akisifia vitu akisema “una vitu vizuri sana, u msafi pia meza yako inavutia. Tutarudi siku nyingine.” Nilitabasamu tu nikisema “nashukuru sana, karibuni sana.” Sasa alinipa pesa ambayo natakiwa kumrudishia elfu tano. Nikaweka pesa ile nyingine nikaanza kumuomba jirani, huyu kaka alinitazama na kusema “usijali dada, baki nayo tu. Tunashukuru kwa huduma yaoo nzuri.” Uwiiii!!, vile nilikuwa na shida na hela, vile huyu kaka anatabasamu, anaongea mimi ndiyo sijui nichanganyikiwe au furaha izidi. Nilijikuta natabasamu, ukisikia baba kuna jambo nilikuomba, na nimeona umelijibu ni hili langu mwenzenu. Mungu amenipa kicheko. Sikuwa hata nimeuza lakini naona ndani ya muda mfupi nimeuza tena pengine hata ya aliyeanza asubuhi. Nilitamani hata nimpigie simu mama yangu, ila hana hata simu. MY HEART BEAT:07 Natamani uone macho ya jirani zangu lakini sijali kama ambavyo wao walikuwa wakiuza mimi sijali. Nilikaaa nikimshukuru Mungu kwaajili ya hawa malaika. Kwa macho ya kawaida ni kama wateja, kwangu hawa walikuwa ni malaika. Nilijikuta kila nikiwawaza natabasamu tu. Na tangu wao walipotoka tu biashara ndiyo kama ilifunguka, sio kama nauza kama wale walivyobeba vingi, ila nauza uza tofauti na mwanzo. Basi Hope mimi nikikaa namkumbuka yule kaka, sijui hata ilikuwa inatokea tokea vipi ninajikuta sura yake inanijia kwa kasi sana na natabasamu tu. Mtu ndiyo kwanza nimemuona, sijawahi muona, simjui hanijui lakini sasa najikuta natabasamu tu muda wote. Sikuwa nataka kuchelewa sana kwasababu ya mama yangu nyumbani. Furaha nayo haikuwa inakoma kabisa. Niliweka eneo langu sawa. Nikamuaga rafiki yangu na kuanza safari ya kurudi nyumbani tena nikiwa sasa kawaida sina hata hasira. Nikiwa njiani nilikumbuka mdogo wangu amezungumzia nyama, na mimi nina elfu tano ambayo nimeachiwa na yule kaka baada ya kumuhudumia. Sijui yule ni nani yake ila ndiyo aliniachia elfu tano. Nikaona sio mbaya mama yangu, kaka yangu leo wakala vizuri. Ninakumbuka niliingia buchani na kununua nyama. Nilitoka nikiwa natabasamu. Nilipofika nyumbani tu, mdogo wangu ambaye huwa tu napenda kumwita kaka kama heshima yake, aliponiona tu alisema “bora umerudi mapema dada, nataka nitoke mara moja kesho nina mtihani nikajisomee na wenzangu hapo jirani.”
Nilitabasamu na kumuuliza “eenh, leo ugali au wali?” Akacheka akisema “masihara hayo dada, acha kufananisha wali na ugali.” Nikacheka nikisema wewe tena na wali. Basi nilimtaka asichelewe, mimi Nikaingia ndani, kuchungulia chumbani kwa mama yangu, mama alikuwa tayari amelala. Na nilitabasamu tu na kuvuta pumzi. Nikaingia ndani ya chumba changu na kuanza kupiga mahesabu zile pesa ambazo nimefanya kazi leo huku nikitenga dawa, mahitaji muhimu, biashara na kidogo kwenye kibubu kwaajili ya mdogo wangu shule. Nilipomaliza nilivuta pumzi ya uchovu nikisema “Mungu nisaidie.” MY HEART BEAT:08 Baada ya hapo sasa ndiyo nikabadili nguo na kutoka kuelekea nje. Hapo nje hakuna hata sehemu ya kupikia ni unawasha tu jiko la mkaa na kuweka sehemu nzuri ambayo naweza kukaa nikapika na mimi napenda sana kukaa mlangoni ndiyo nipike. Niliandaa mboga nikaweka jikoni huku kaka yangu akiwa tayari amefanya kazi zingine kama kusafisha vyombo na kufua. Ninampenda ni kaka ambaye anaelewa hali halisi ya nyumbani. Mimi nikaendelea tu na shughuli zingine ambazo najua fika asubuhi zitanisaidia kuwahi kazini endapo nikizifanya kabisa. Huwezi kuamini baada ya kurudi jikoni naanza kuunga mboga si nikawa kama nipo sokoni yule kaka amekuja sasa ndiyo anauliza kuhusu vitu vyangu. Najikuta natabasamu. Kisha najishangaa nikisema “Hope una shida gani wewe mbona unatabasamu hivyo lakini.” Nilikuwa naona kabisa ninaelekea kuwa mjinga kisa mtu ambaye simfahamu. Kama hujawahi kukutwa na hali kama yangu huwezi kunielewa ila huwa inachekesha sana, kwa mara ya kwanza ndiyo naona kumbe mtu unaweza kushindwa kujizuia kutabasamu kabisa tena ukawa unafanya vitu kama mjinga. Nilipika nikiwa nina furaha sana, nilikuwa na furaha. Sijui hata ilitoka wapi ni kama moyoni nimetua mzigo mkubwa sana. Sasa nikawa nimemaliza ndiyo narudisha vitu mahali pake, wakati naingiza chakula nikasikia mama yangu anaita “mrembo wangu, mrembo wangu!!” Nikatabasamu na kumjibu “mama yangu, umeamka kumbe.” Nilikuwa sitaki hata ajibu, nikawa naelekea chumbani kwake. Mama alinitazama usoni, nikawa natabasamu tu na aliniuliza “mbona kunanukia sana, kuna nini leo?” Nikacheka sana nikisema “tatizo lako mama Hope umezoea siku kuu mpaka siku kuu.” Mama alitabasamu tu, kisha nilisema “subiri mama namalizia kazi nakuja sasa hivi nikupe chakula kisha unywe dawa muda umeenda sana.” Mama alitabasamu tu. Ninakumbuka niliingiza ndani kila kitu na baada ya muda nikamuandalia mama chakula na kisha nikaingia chumbani kwake. Alipoona sahani tu mama alitabasamu akisema “mwanangu leo umeua mtaji unajua chakula kizuri hivi?” MY HEART BEAT:09 Nikatabasamu nikasema “kwaajili yako mama yangu, ule vizuri upate afya, si unajua nakupenda sana eenh. Na kuhusu mtaji usijali sijatumia mtaji sana leo.” Mama alinitazama na kusema “mwanangu, nashukuru sana kwasababu hujanitupa mama yako. Najua kuuguza kazi sana, najua bado umri wako mdogo unachoka, lakini bado umenichagua mama yako kwa nguvu zote. Namuomba Mungi hapa kitandani, ugonjwa wangu usiwe mzigo kwenu wanangu, natamani sana siku niamke hapa, nifanye kazi kwa bidii ninyi mpumzike.” Nilimtazama mama kwa hisia, kisha nilimshika mikono yake nikisema “wewe ni mama yangu, mama umenizaa mimi sijakulipa chochote. Wewe ni Mungu wangu wa pili kwenye hii dunia. Baraka zangu zipo mikononi mwako. Wewe sio mzigo mama, wewe ni mama haijalishi tunapitia nini. Usiseme maneno haya tena unaniumiza. Jambo kubwa na zuri kuliko mama niombee, niombee sana mwanao ilo walau tuvuke hatua kadhaa mbele. Nakupenda hunisumbui kitu, na huu ni wajibu wangu kama mtoto kwa mama yangu. Sawa mama yangu?, na utapona tu Mungu ni mwema sana.” Mama alinitazama kwa upendo sana na kutabasamu. Kisha nikachukua sahani kwa upole kwa maana maneno ya mama yalikuwa yameingia moyoni kama mtoto namuonea huruma sana. Nikamlisha kijiko cha kwanza. Mama alinitazama akisema “mwanangu vya kurithi vinazidi ndiyo chakula kitamu namna hii.” Nilitabasamu na kusema “acha utani mama wewe unapika unajua, wewe fundi sana. Nikifikia uwezo wako nafungua mgahawa.” Mama alicheka tu, na mimi nikawa naendelea mlisha huku natabasamu. Mama akawa tu anakula huku ananitazama. Baada ya kumaliza wakati nachukua dawa mama yangu aliendelea kunitazama, akameza dawa na kisha akaita “Hope mwanangu!!!” Nilimtazama na kusema “abee mama yangu.” Mama yangu alisema “nashukuru mwanangu, Mungu akufungulie ridhiki.” Nikatabasamu nikisema “asante mama, maombi yetu ya leo mchana Mungu amejibu, sijaamini hata nimeuza sana leo.” MY HEART BEAT:10 Mama alitabasamu akisema “ndiyo hilo tabasamu naona usoni au kuna kingine mwanangu?” Nikajikuta nacheka nikisema “ila mama, unachunguza mpaka tabasamu si ndiyo nilivyo mama.” Mama akasema “mmh mwanangu, wewe wangu ujue haya niambie nini siri ya hilo tabasamu?, nyuma yake kuna nini?” Nilicheka nikisema “hapana mama, nimefurahi sana leo. Si unajua mchana nilikata tamaa, lakini Mungu amefanya.” Mama alitabasamu akisema “tuendelee kusali tu mwanangu.” Kabla hata hatujaendelea, kaka yangu mdogo alirudi akisema “dada njaaa, njaa inauma kama nini?” Nilitazamana na mama nikisema “huyu ndugu yangu njaa haiwezi kabisa yaani na hapo akijua nilichopika utasikia tu mama.” Mama alicheka akisema siwawezi. Kweli nikafika sebuleni, ile kuandaa tu, mdogo wangu aliuliza kwa hamu sana “kitu cha wali nyama?, waoooo ndiyo maana nakupenda mama, wewe ndiyo mama yangu mimi.” Nilijikuta nacheka nikisema “mama unasikia mwanao huku, nishakuwa mama yake tayari. Linapenda kula toto lako.” Tulisikia mama anacheka kwa furaha na hii kwetu ilikuwa ndiyo kila kitu. Mimi na ndugu yangu tulikula pamoja kwa furaha baada ya kumaliza kaka sasa alianza kwa kusema “nimeshiba sana, eenh Mungu mpe dada pesa kila siku tule Kama leo.” Mama kwa chumbani alijibu “ombi lako limekataliwa.” Tukajikuta tunacheka, ndipo mdogo wangu alisema “dada nashukuru sana kwa chakula, Mungu akubariki sana. Nakuombea na Nakupenda sana.” Nilitabasamu, akatoa vyombo na kwenda safisha, nami nikasafisha ndani. Tukaingia chumbani kwa mama tukasali Pamoja na kisha kila mmoja aliingia chumbani kwake. Nilipokuwa chumbani, nilijitupa Kitandani kama unione vile, nacheka cheka tu kinachonichekesha najua sasa, kila tu nikimkumbuka yule mkaka ndiyo najikuta chizi wa kujitegemea. Kesho yake nilifanya majukumu yangu kama kawaida, nilihakikisha mama namuacha salama mimi kazini. MY HEART BEAT:11 Nilitamani sana kumuona yule kaka, lakini haikuwa rahisi maana amenunua vitu vingi sana. Hivyo sio rahisi kurudi na sijawahi kumuona kabla. Hivyo siku hii iliisha natazama huku na kule na hakuja. Niliishi hivi kama wiki, hata nilikata tamaa kabisa ya kumuona. Nakumbuka hata siku moja Nilirudi nyumbani roho inauma sijamuona eti. Kiasi mama yangu aliniuliza “mbona umepoa sana siku mbili hizi kuna tatizo?” Nilimtazama mama na kusema “hapana mama, hakuna tatizo.” Mama alinitazama na kusema “lolote linalokupa wakati mgumu, ita Mungu katikati yake, unaweza kuona hafanyi kitu lakini ndiyo tayari amefanya kwasababu kuna wakati Mungu anakupa kile anaona ni linafaa kwa wakati huo.” Nilimtazama mama na kusema “unajua Mama una imani sana, sasa mfano hapo kitandani kwa maombi yako si ungekuwa umepona?” Mama alitikisa kichwa na kusema “temea mate chini mwanangu, kamwe usirudie kusema hivyo. Sikuwa hivi mimi, na jambo la muhimu nipo, tunaongea, tunabadilishana mawazo hata ningekuwa siwezi lolote unaniona kila siku ni jambo la kushukuru Mungu. Ni kweli sijaamka kitandani lakini pengine hii ndiyo njia sahihi sisi kuishi na inatuweka karibu zaidi na Mungi. Huwezi jua kulala kwangu ndiyo sababu maisha yetu yapo hivi sasa, usikate tamaa upesi hivyo, Mungu yupo na njia za Mungu hazichunguziki. Unanielewa mwanangu.” Nilijikuta hata najisikia aibu, nilisema “nimekosa mama, naomba nisamehe.” Mama alisema “kuwa sawa mwanangu, nakuomba.” Nilitabasamu. Tulifanya ratiba za kila siku kisha nikaenda kulala. Nilikuwa nasubiri tu muujiza nimuone tena huyu kaka nifurahi. Wiki kama mbili hivi zilipita, ninakumbuka sana. Siku hii tena nilimuona huyu kaka mbele ya meza yangu. Nilipomuona nilijikuta natabasamu. Alinitazama pia na kutabasamu akisema “tumerudi tena.” Nilitabasamu kisha nikamsalimia yule baba “shikamoo baba.” MY HEART BEAT:12 Huyu baba alisema kwa tabasamu “marahaba mwanangu, una vitu vizuri sana. Tuchagulie kama ile siku.” Haraka haraka nilianza kuwapangia, huku kijicho cha wizi nikimtazama yule kijana ambaye naona raha kumtazama. Na yeye ananitazama ana tabasamu tu. Safari hii waliongezea na vitu vingine te a basi ikawa raha moyoni kwanza napata hela, na nyingine nimemuona tena leo nasikia sauti yake akiniongelesha sana Nasikia raha sana. Walinunua vingi sana, nilifurahi. Kisha walibeba mfuko kila Mtu wake, wakalipia na wakaanza kuondoka huku mimi nikiwa natabasamu tu. Baada ya sekunde nikainama kuweka pesa vizuri, ile nainuka tu nashuhudia yule kijana ambaye ananifanya mimi namtazama ameanguka chini, tena ameanguka kama mzigo, watu wa karibu naye wanapiga kelele na kuanza kukusanyika pale, namuona yule baba akihangaika kuomba watu wasogee pembeni, macho yangu yalinitoka, mshangao ulikuwa sio wa kawaida, akili yangu haikuwa pale tena, nilijikuta ninakimbia, ninakimbia kwa nguvu zangu zote, walau nikampe msaada huyu mwanaume ambaye ananisumbua, nikafika mpaka eneo la tukio, baada ya kumuona, nilishindwa kujizuia machozi yalinitoka, machozi yalinimwagika na kujikuta namsogelea karibu zaidi, nikapiga magoti yangu na kuweka kichwa chake juu ya migui yangu. Tena huku machozi ya woga na huruma yakinitoka, alikuwa akitaabika sana pale chini MY HEART BEAT:13 Alikuwa anajipigapiga kwa maumivu, kwa mateso, kwa kuumia sana, alikuwa anatokwa mapovu mdomoni mpaka machozi, yaani kila ninapotaka kuelezea namna nimemuona napata ganzi, vile anateseka mpaka mkojo unamtoka. Mimi nipo nimemshikilia nasema “Mungu nakuomba msaidie, msaidie kijana wako, usikubali awe hivi kwenye haya maisha yake yote, muhurumie, mfanyie pumziko, anateseka Mungu, ni nini hii, Mungu nakuomba fanya kitu leo.” Oooh!!? Wapiii ni kama vile nazidisha, yaani ndiyo anazidi kujipigapiga, vile mimi nimezoea kumuuguza mama yangu wala sikuwa naona shida. Watu wanaogopa, naona vile wanashangaa. Tena tunasikia maneno yap kabisa, huku yule baba anayekuwa naye na yeye akionekana kumsaidia huyu mwanaume. Aiseee!!, kuna sababu ya kumshukuru Mungu sana kwa namna umeumbwa, kwa jinsi ulivyo wewe na afya yako. Kuna maradhi yanaumiza, yanadharirisha, yanatia aibu. Ndiyo nateseka na mama yangu, lakini huyu mwanaume anateseka, mama yangu anaumwa ni kweli ila hapitii haya. Nikiwa pale nimepiga magoti, nilikuwa nasikia watu wanavyosema “hiki ni kifafa, kifafa kabisa hiki. Maskini tena mwanaume mzuri huyu, inakuaje tena anakuwa na kifafa jamani.” Kila nilipokuwa nasikia maneno haya namtazama napata uchungu moyoni. Uso wake naubeba mimi, unajua nawaza mengi mpaka nachangangikiwa. Natazama suruali yake machozi yananitoka huku nikisema “Mungu wewe watosha, nashukuru sana kwaajili ya afya yangu.” Mwanaume huyu akawa anapoa, tena alikuwa ameshikilia mkono wangu, anapoa taratibu na hapo ni baada ya dakika kadhaa za kutosha kupita. Yule baba alikuwa karibu sana na huyu mwanaume kuhakikisha anakuwa sawa. MY HEART BEAT:13 Nakumbuka vile huyu kaka macho yake yalikuwa yanazunguka kutazama lile kusanyiko la watu kisha kunitazama mimi vile nimeweka kichwa chake kwenye miguu yangu. Hakufanya kitu kingine chochote zaidi aliyafumba macho yake tena kwa maumivu makali maana machozi tu ndiyo yaliyokuwa yanamtoka. Nilikuwa naelewa vile anajisikia. Hapo chini kila walichonunua kimemwagika na kiasi ndiyo vimebaki kwa mfuko. Baba huyu alisimama na kusema “samahani, tunaomba nafasi kidogo ili tuweze kuondoka hapa.” Huku minong’ono ikiwa inaendelea, huyu baba alinitazama na kutabasamu kwa uvivu sana. Akaanza kumuinua huyu mwanaume kwenye miguu yangu. Na mimi ikabidi nisaidie maana haikuwa rahisi kumuinua. Tuliweza kufanya hivyo pamoja. Nilimshika upande kwa kushoto, na baba kulia yeye akiwa katikati yetu. Kisha kijana mwingine alijitolea kubeba ile mifuko na baadhi ya vitu vyenye unafuu. Tulifika mpaka nje kabisa ya soko kwa taabu sana. Tulipofika tulielekea upande ambao tulikutana na gari. Sikuwa hata nimezingatia gari yenyewe. Tulipofika baba alifungua gari na tukasaidiana jamaa aingie kwa gari na aliyeleta mifuko na yeye akaacha pale na kuondoka. Mimi Nilipohakikisha amekaa vizuri, hawezi hata kunitazama usoni. Nilifunga mlango wa gari nikawa namuaga baba yule nikisema “pole sana baba, kijana wako atakuwa sawa. Tumuamini Mungu tu kwenye hilo.” Huyu baba alitabasamu, na kisha aliniuliza swali “unaitwa nani?” Nikatabasamu, nikimtazama usoni na kumjibu “Hope, naitwa Hope.” Baba huyu alisema “mimi na kijana tunashukuru sana, sina namna ya kuelezea sana shukrani yetu lakini umekuwa msaada sana kwetu siku ya leo. Mungu wa mbinguni akubariki sana. “ MY HEART BEAT:14 Nikatabasamu tena na kusema “nashukuru sana baba. Asante.” Huyu baba alisema “asante sana, natumaini tutakutana tena hivi karibuni.” Nikamtazama na kumjibu tu “Karibu.” Alinitazama, mimi nikawa natabasamu huku napunga mkono wa kwaheri kwa maana biashara yangu nimeacha peke yake na hela sijapanga vizuri. Nilirudi ndani ya soko, ile nimerudi tu. Ile nimerudi nakuambia watu wananishangaa kila mmoja akisema lake, nakumbuka sana maneno yao “Hope wewe kiboko wenzako tunaogopa wewe unatoa msaada vile. Unajua anaweza kukufia yule. Kile kifafa chake sio cha kawaida nakuambia sio kawaida kabisa. Vipi unawafahamu wale kwani?” Mimi nikawa nawatazama tu natabasamu, huku wengine wakinipa hongera kwa kuwa jasiri lakini ili halikuwa lengo, msukumo ambao niliupata mimi mpaka kumsaidia huyu mwanaume sijui ni wa namna gani. Nikisema hapa nikuambie ninavyoumia ndani ya moyo wangu, baada ya mwanaume nimesubiri wiki mbili mpaka kumuona tena akianguka mbele yangu, na kuumwa vibaya sana oooh Moyo wangu ukatika vipande vipande. Ninaumia kuliko kawaida, ninajisikia vibaya kuliko ninavyopaswa kujisikia. Utasema huyu naye anauguza mama yake mbona anacheka tu. Ni mama yangu, ninaumia sana kumuona pale kitandani, lakini huyu mwanaume ameniumiza sana. Ukiniuliza Hope kwanini huyu mwanaume anakuuma hivyo, sina jibu, sina kabisa ni kitu kipo ndani ya moyo wangu na siwezi kabisa kuzuia, siwezi. Nilipita mpaka kwa meza yangu, nilijitahidi niweke mambo sawa. Huwezi kuamini, kabisa huwezi nilijikuta vile nimekaa nimeinamisha kichwa changu chini nimekumbuka maumivu ya mama yangu, nimechukua maumivu ya huyu kaka mpaka kunitazama usoni hawezi nimejikuta ninalia kilio cha maumivu sana, nimejikuta ninaumia kiasi kwamba nashindea hata kujizuia maumivu yangu. MY HEART BEAT:15 Mpaka mteja akaja pale ndiyo mimi kufuta machozi na kuinuka, aliponitazama aliniambia tu “pole dada, jitahidi upate dawa.” Nilimwambia kwa upole “nashukuru sana, karibu.” Basi nikamuhudumia na nilipo malizana naye aliondoka. Kila nikikumbuka kuhusu yule mwanaume na alivyo fadhaika ninajiona nina siku mbaya sana, nina siku ambayo siwezi kuivumilia kabisa. Wakati nikiwa natafakari mawili matatu, nimekosa raha kuna mama meza ya mbali kidogo machp yetu yaligongana. Na kisha aliniita kwa mkono. Ilinibidi nisimame na taratibu nitembee uelekeo wake. Mpaka nilipofika kwake alinikaribisha na kisha aliniambia “Hope, una moyo mzuri sana. Watu kama wale wanaogopwa.” Nilitabasamu tu, kisha alinitazama na kuniuliza “unafahamiana na watu wale?” Nilimtazama nikiwa naendelea kutabasamu tu huku nisijue kitu cha kujibu, huyu mama hakuwa hata nauvumilivu. Alinishika mkono akisema “nakuuliza kwa nia njema kabisa mwanangu, kuna mama nina mfahamu mtoto wake alipatwa na kifafa tena cha kuzaliwa nacho. Alihangaika sana, ila huyo binti yake ni mzima sasa. Pengine tukimfuata anaweza kutuambia alitumia nini mpaka mwanaye akapona, au alifanya nini binti yake akawa sawa.” Nilimtazama na kumuuliza “ina maana kumbe huu ugonjwa unatibika.” Alinitazama usoni na kusema “sina hata jibu mwanangu, maana dunia yenyewe ina mambo mengi lakini na utu uzima wangu huu huwa naona wengi wanatumia dawa za hospitali na wengine za asili. Wapo wanaokaa vizuri na nimeona wengine wakipoteza maisha katika hali kama ile.” Nilishangaa nikiuliza “kwahiyo anaweza kufa akiwa katika hali ile?” Huyu mama alisema “Hope, tusiongelee sana hilo. Kama ni mtu mnafahamiana basi ongea naye akikubali utaniambia tuanze kumpeleleza huyo mama.” Nilimtazama na kusema “nashukuru sana, nitarudi tena kwako mama, Ubarikiwe sana kwa kujali. Nashukuru.” Alinitazama tu nami nikarudi kwa meza yangu. MY HEART BEAT:16 Haki ya Mungu sikuweza kukaa sana, maneno ya huyu mama kama unaweza hata kufa ndiyo yaliyozidi kunichanganya. Huwezi kubali kuwa huyu mtu ni mteja tena ni wa mara mbili lakini ninamuonea huruma kama vile tuna uhusiano wowote ule labda rafiki, ndugu au vyovyote. Hata jina lake tu simjui ila ananisikitisha sana. Nilishindwa mwenzenu, nikafunga ofisi yangu tena hii siku hata sikuwa natembea haraka. Taratibu nikawa natembea huku nikiwa na vitu kwaajili ya kuandaa jioni. Nilifika mpaka nyumbani nilikuta kaka yangu na mama wakipiga story chumbani. Baada ya wao kuniona kaka ndiyo aliuliza “mapema sana leo, salama dada yangu.” Nilimtazama kwa tabasamu nikisema “nimechoka sana leo, nimeona niwahi tu kupumzika.” Mama yangu alinitazama na kuuliza “upo sawa lakini binti yangu?” Nikamtazama na kumjibu “kabisa mama, niambie umeshindaje, huyu lastborn wako amekupa vizuri chakula.” Kaka yangu akacheka akisema “hujui balaa langu wewe muulize mama alivyoshiba kidogo nimsongee ugali.” Nikacheka lakini mama yangu hakucheka na badala yake aliniuliza “mwanangu, ulikuwa unalia?” Nikamtazama mama kwa mshangao, hata yeye akamwambia kaka yangu “kaka, tupishe kidogo niongee na dada.” Kaka yangu akasema “siendi mbali nipo kwa jirani hapo mkimaliza tu dada uniite.” Nikatabasamu, na yeye akawa anatoka akisema “mazungumzo mema mama zangu.” Nikatabasamu. Kisha nikamgeukia mama nikisema “hapana mama, leo nimekuwa tu na siku mbaya mama.” Mama aliniuliza tena swali “Siku mbaya kwasababu gani?, hujauza pia leo ndiyo unalia?” Nikasema tena kwa upole “hapana mama wala hata sio hivyo. Lakini….” MY HEART BEAT:17 Mama alinitazama akitabasamu na kuniuliza “lakini nini binti yangu?” Nikavuta pumzi na kusema “mama yangu, sio jambo kubwa sana ila leo kuna mteja wangu ameanguka sokoni.” Mama akaniuliza “kuanguka?, ameangukaje sijaelewa.” Nilimtazama mama na kusema “Kifafa mama, anaumia sana, anateseka sana nimemuhurumia sana.” Mama alinitazama na kusema “maskini!!, ni huwa wanajisikia vibaya sana, pia watu wa hivi wengi hawana kujiamini tena maskini, ni mwanamke au mwanaume?” Mimi nikamtazama nikisema “mwanaume mama, ukimuona utamuhurumia.” Mama alisema “tayari nimemuhurumia. Nakumbuka shule kuna mtu aliwahi kufariki kwasababu ya tatizo kama hilo.” Nikamtazama mama nikisema “weee mama usiniambie?” Mama alinitazama na kusema “ni kweli, aliumwa kawaida lakini baadaye alipigwa na kifafa hakuweza tena mpaka chaga ya kitanda ilivunjika wakati ana kata roho.” Natamani mama amgejua namna ananiumiza roho yangu, nazidi muhurumia. Uso wangu ulisema yote, mama yangu aliendelea akisema “lakini ugonjwa huohuo wapo ambao wakihangaika wanapona na wapo ambao ndiyo maisha yao. Ni Mungu Tu mwanangu ndiyo anajua siri ya maisha yetu. Sasa kwanini unajisikia vibaya mwanangu ni rafiki yako?” Nilimtazama tu mama, mama yangu alinishika mkono na kusema “una roho nzuri sana mwanangu. Upendo wa ndani ya moyo wako ni mkubwa sana. Mungu akujalie moyo huohuo miaka yote mwanangu. Kwasasa hupaswi kuwa hivyo, zaidi uwe unamuombea mteja wako, pia msisitize kusali na usiache kumtia moyo maana asilimia kubwa wamepoteza tumaini, hawana kujiamini tena. Najua unaelewa ninachosema.” Nilimtazama mama na kusema “nimekuelewa mama, wacha nikapike sasa.” Mama alitabasamu tu. Kiukweli Mimi niliingia unyonge hata kuzuga siwezi. MY HEART BEAT:18 Nilibadilisha nguo, nikaweka mambo sawa nikatoka na kuanza kupika. Kaka yangu na yeye alirudi na kuja jikoni kunipigisha story za hapa na pale walau nikawa nacheka sana . Pamoja tuliandaa na mimi nikaingia mlisha mama, kisha tukala na sisi japo mimi sikuwa hata na hamu. Hata kaka yangu akaniuliza “dada huli leo?” Nilitabasamu nikisema “nasikia vibaya tu nitakula lakini.” Kaka yangu alinitazama kwa huruma na kusema “Mungu afanye kitu, hupaswi kuumwa dada yangu nakuomba unywe dawa.” Kauli ya kaka yangu ilinifanya niumie, inaonesha namna gani ananitegemea hatamani hata dada yake niumwe. Nilimtazama na kusema “mdogo wangu kipenzi, sitaumwa. Daima nitakuwa mzima kwaajili yako na mama mpaka na wewe uweze jitegemea sawa kaka wa mimi.”
Alitabasamu akisema “nakupenda sana dada yangu.” Na mimi nikajibu “nakupenda sana kaka yangu.” Kisha tuliendelea kula kwa upendo na furaha. Baada ya hapo kila mtu alifanya kazi yake, tukaingia kwa mama kusali na kisha kila mmoja alikamata njia yake kwenda kulala. Nilipoingia chumbani, baada ya kuweka kila kitu sawa, sikuwa naweza kulala kabisa. Nilijilaza kitandani kwa unyonge sana nawaza kweli kuhusu hili suala la huyu mwanaume kuanguka mbele ya macho yangu. Nilikuwa namuhurumia kwanza, pili kwanini yeye ambaye mimi ninamfikiria sana ndiyo awe na kifafa, kwani lazima awe yeye. Nilikumbuka namna amenishika mkono wangu lakini bado hakuweza kunitazama hata usoni kwa aibu, hakuwa anaweza kunitazama kabisa. Alikuwa amefedheheka na pengine labda asirudi tena eneo lile kwasababu ya watu kukumbuka lile tukio. Hakika niliwaza mengi kumuhusu huyu mwanaume mpaka pale nilipo amua kulala. Niliamka tena na mapema na kufanya kila kazi yangu, nilifanya kila kitu kwaajili ya familia yangu na kuagana na mama yangu kama ilivyo kawaida. Hakuna mtu wa kumuacha naye lakini lazima pia nitafute pesa hivyo mpaka mdogo wangu atoke shule ndiyo walau anapata mtu wa kumuangalia. Tumezoea wenyewe maisha yetu. MY HEART BEAT:19 Siku hii sokoni kila mtu alikuwa na mambo yake kuhusu suala la yule kaka lilishapita kabisa. Hakuna mtu alikuwa anawaza isipokuwa mimi tu maana sikusikia wakiliongelea labda huko nyumbani kwao wakisumuliana kuwa kaka mzuri ameanguka kifafa mpaka amejikojolea unajua watu tena. Lakini kwa sokoni pale hakuna habari kama hizi wala hakuna mtu yeyote ambaye anazungumzia. Maisha yaliendelea hivyo hivyo kwa kudunduliza ili mradi mkono unaenda kinywani. Ninakumbuka ni zaidi ya mwezi ulipita nilipokea simu kutoka kwa mmiliki wa ile meza yangu ya sokoni na wakati huu mama yangu nilikuwa nikimlisha. Aliniambia maneno haya “Hope ndugu yangu, najua ni haraka na tofauti na makubaliano lakini biashara niliyotegemea itanipa faida imekuwa ngumu sana. Hivyo naomba tu unirudishie meza yangu niendelee na kazi. Kuhusu kama una vitu pale basi tutapigiana mahesabu.” Sikuwa naliona hili mapema hivi, nilijiiuta machozi yananitoka kabisa, nilijikuta natokwa na machozi nikisema “imekuwa ghafla lakini, hatukuwa tumekubaliana hivi?” Ni kama nilimkwaza sana na swali hili, alinijibu “kwahiyo unataka nifanye nini, meza si ni yangu nina haki yangu pia. Ninakuelezea bado huelewi kwahiyo unataka tu nikae bila kazi wakati nina meza yangu sokoni.” Nikamtazama mama kwa maumivu nikifuta machozi yangu na kusema “samahani sana, naomba nisamehe sana basi hakuna shida kuhusu hilo.” Hakunijibu hata alikata simu. Nilijikuta ninashusha pumzi yangu ndefu sana.Nilisahau hata nilikuwa namlisha mama yangu, niliinuka na kutaka kutoka. Nilipofika mlangoni mama yangu kwa huruma aliita “binti yangu!!!” Nikasimama nalia huku nawaza nitaishi vipi bila kazi walau sokoni ukikosa kabisa utabeba mboga, viungo na sasa natakiwa kurudisha maisha kabla ya hapo nakumbuka sasa narudi kulekule. Kwahiyo ule uchungu moyoni, ninaumia, ninashindwa kuzuia machozi yangu kabisa. Nilirudi kwa mama yangu, mama alinitazama usoni na kuniuliza “kuna nini mwanangu?” Nilijikuta ninamkumbatia mama yangu pale kitandani kwake na kuanza kulia nikisema “mama, sina kazi tena. Mwenye meza yake anahitaji. Sijui hata nitafanya nini mimi mama.” MY HEART BEAT:20 Ninamfahamu mama yangu, ni wazi hizi habari ni mbaya sana kwake, lakini atafanya nini mama yangu, hana la kufanya zaidi anatakiwa kunitia moyo. Niliona hayo kwenye macho yake alishindwa hata kuongea baada ya mimi kuinuka. Alisema “usilie basi mwanangu, Mungu wetu ni mwaminifu sana. Hatuwezi shindwa kuishi. Jinenee mambo mazuri mwanangu, milango mingine ya baraka itafunguka na mambo yatakuwa sawa. Mungu hawezi kutupitisha mahali hakuna njia kabisa, hata kwa kupambana sana lazima tupite. Kuwa imara mwanangu.” Nilimtazama mama na kusema “mama, nakuelewa, imekuwa ghafla sana.” Mama alisema “usishindane na mwenye nacho mwanangu, mpe eneo lake, mpe meza yake ipo siku hata kama usipopata kama yake utapata pakusimama hata kama sio pazuri kama pale ila patakuwa kwaajili yako.” Nikachukua sahani tena ili niweze kumlisha. Mama alinitazama tu usoni na kutikisa kichwa, ndiyo hii habari haikuwa nzuri, mama ananihurumia sana. Nikampa dawa na kumuaga siku hii hata kusali sikuwa naweza kusema kweli.Nilipofika chumbani nilipanda kitandani na kulala, nikawa nageukia upande huu nalia, nageukia huku nalia, Mara nikae, Mara kichwa kiwe miguuuni na miguu iwe upande wa kichwani. İli mradi tu mawazo maana kuanzia mama mpaka mdogo wangu kila kitu ni mimi. Baada ya muda nilisikia mdogo wangu akibisha hodi, alipoingia tu baada ya kumruhusu alikuwa anatembea taratibu akiita “dada, unalia hivyo?” Ndiyo Nikazidi kuumia, nikamkumbatia mdogo wangu na yeye alinikumbatia akisema “najua ni kwaajili yetu unapata taabu, dada niambie nifanye nini nikusaidie.Niambie nifanye nini utapunguza uchungu moyoni. Mama ameniambia kila kitu.” Nilimtazama na kusema “mama hakupaswa kukuambia hili, sio kwamba tunakutenga. Lakini wewe kazi yako kusoma tu. MY HEART BEAT:21 Usijali kuhusu mengine mimi ni dada nitapambana. La kufanya wewe ni kusoma tu. Niahidi utajiweka kwenye masomo tu na kuwa kijana mzuri.” Alitabasamu, akafuta machozi na kusema “Nakuahidi dada, na nakuombea sana dada kıla mazuri yaje kwako.” Nilimkumbatia Kisha nilisema “haya kalale sasa kesho uwahi shule.” Alinitazama akitabasamu na kusema “sali.” Nikatabasamu pia nikisema “sali.” Ni tabia ya ndani kwetu kukumbushana ibada. Alipotoka tu na mimi nilienda kwa mama, lengo kumwambia mama asimshirikishe mdogo wangu kuhusu matatizo atashindwa kusoma. Mama alitabasamu na kusema “ninachokupendea unajali sana mwanangu, nisamehe mama yako nilichanganyikiwa.” Nikamtazama na kusema “ulikuwa unalia mama?” Akatazama kwingine na kusema “nimechoka sana mwanangu, naomba ukalale.” Nilimtazama tu mama yangu na kutii ingawa iliniuma sana. Nakumbuka sıkılama vizuri, na kesho yake si kwenda kabisa sokoni. Badala yake nilipomalizana na wakati najiandaa kutoka nilipokea muamala wa pesa ndogo sana kutoka kwa mwenye meza yake elfu 20 tu. Nilitamani kuuliza nikakumbuka mama alivyo sema nisishindane na mwenye nacho. Nilisema tu “Mungu nisaidie.” Niliamka na kuanza kupita mtaani, sikuanzia mtaa wangu. Nilipita mitaa mingine, naomba kazi hapo kufua, kufanya usafi, kupika, kuosha vyombo. Mungu si athumani mwanzo mgumu lakini wapo walioniamini mama mdada alikuwa mjamzito nikamsiadia kazi, akanilipa nikaondoka akasema baada ya kushinda kesho kesho kutwa nirudi, nikapata na sehemu nyingine. Inalipa ingawa sasa huwezi kwenda sehemu nyinyingi.Na hii sasa ndiyo ikawa kazi yangu mpya nikiwa nimepoteza kabisa tumaini La kukutana na yule mwanaume.Nilikuwa najitahidi kadri niwezavyo nyumbani kipatikane kitu. Ingawa sio kila siku napata kwahiyo nikipata natunza ni miezi kama mitatu nilifanya kazi hii kwa uaminifu kabisa. Nikirudi nyumbani nachoka hoi, nitafanyaje tena na ndiyo ukubwa. MY HEART BEAT:22 Mungu muacheni aitwe Mungu, akitaka lake hata iweje lazima iwe tu. Ninakumbuka sana hii siku, sikupata kazi kabisa. Nilitembea sana hata nikachoka mno.Na haya yote ni kwaajili ya mama, anatakiwa kurudi hospitali, anatakiwa dawa na mimi lazima nihangaike. Başi nilirudi kwa kuchelewa nikapitia mahali kuweka pesa ya upatu nikawa narudi nyumbani. Sasa nimefika nyumbani, palikuwa pametulia sana. Nilianza kuita nikiwa mlangoni, “mama!!!, mama!!, upo sawa?” Mdogo wangu alitoka na kusema “dada una mgeni.” Nikauliza kwa kushangaa “mgeni, yupo wapi mbona nje hakuna mtu?” Mdogo wangu alisema “anazungumza na mama ndani.” Nilishangaa mgeni gani huyo mpaka aongee na mama yangu. Ilikuaje akapita ndani. Nikakaza mwendo kwenda chumbani kwa mama yangu. İle nimefika tu, nashangaa nakutana na yule mwanaume ambaye nilishakata tamaa ya kukutana naye. Alinitazama usoni akiinuka kwa aibu pale kwenye stuli chakavu ambayo alikuwa amekalia. Nilijikuta nashindwa hata kuzungumza, kwa upole maskini kaka wa watu alisema “Hope!!!” Nikamtazama, natamani kuzungumza ni kama nimepigwa na butwaa, alinitazama tena na kusema “samahani sana kwa usumbufu, tunaweza kuzungumza tafadhali.” Nikashusha pumzi na kumtazama nikamjibu “bila shaka, nisubiri nje.” Alitoka bila kusema kitu, Kisha mimi nikamuuliza mama “upo sawa?” Mama alinitazama akitabasamu “nipo sawa kazungumze kwanza na mgeni wako.” Nikatabasamu, Kisha nilianza kutoka. Kabla sijatoka nje kabisa nikajitazama nilivyo. Nilikuwa nimechoka ila nitafanyaje, nikaweka nguo sawa, Kisha nikatoka. Aliponiona alitabasamu, na mimi nilitabasamu. Kisha akanitazama kwa aibu, huruma na upendo. Nikawa natembea taratibu, mpaka nilipomkaribia. Nikavuta Stuli nikampatia na kusema “karibu sana kwetu, umepajuaje huku?” Akatabasamu, Kisha aliniambia “ni story ndefu, ila kufupisha ni kuwa kuna mama amenielekeza hapa.” Nikatabasamu tena na kusema “Karibu sana.” Akaniita kwa upole “Hope!!” Nikaitikia “Abee!!” Akatabasamu na kusema …. 🙌🙌🙌🙌this story Ina kila ladha huwezi juta kusoma 🙌🙌🙌

Post a Comment

TOA MAONI YAKO HAPA

Mpya zaidi Nzee zaidi

Ads related

Smartwatchs