😍😘😘😍
1-------5
Simulizi : Beyond Love (Zaidi Ya Mapenzi) Sehemu Ya Kwanza (chombezotu.blogspot.com)
Tom aliheshimika na kutisha, hakuna mtu aliyechezea shughuli zake kutokana na uhusiano mzuri aliokuwa nao na viongozi Serikalini, akiwa mdhamini wa Chama Tawala. Hakuna mtu ambaye hakumfahamu, kila alipopita watu walionyeshana vidole, alikuwa na marafiki wengi kupita kiasi. Ilipotokea akaa peke yake kwenye baa au hotelini, ndani ya dakika mbili tayari alishazungukwa na watu, kila mtu akiagiza alichotaka kutumia, kwa Tom kulipa haikuwa tatizo, fedha alikuwa nayo. Tabia hii ilimfanya awe na wapambe wengi kila alikokwenda, akilindwa na watu ambao wala hakuwapa kazi hiyo.
Hayo ndiyo yaliwahi kuwa maisha ya Tom, lakini vitu vyote hivyo havikuwepo tena, vilikuwa vimeyeyuka na yeye kujikuta amelala kitandani kwa miaka mitano bila kuwa na fahamu, akiwa amepooza mwili wote isipokuwa kichwa tu! Marafiki wote aliokuwa nao walimkimbia, mwanzoni kila mtu alifikiri angekufa wiki ya kwanza lakini akaendelea kuwepo mpaka mwaka ukaisha, ukaja wa pili, hatimaye wa tatu akiwa hana fahamu. Fedha zote alizokuwa nazo zikiwa zimetumika kumtibu kwenye hospitali mbalimbali duniani bila mafanikio yoyote, hatimaye mke wake mrembo, Mayasa Kamani ambaye kwa hakika walitumbua maisha pamoja wakati wa raha, akaja kumbwaga kwenye Hospitali ya Muhimbili na yeye kuingia mitini akiwa ameuza kila kitu kilichokuwa kimebaki.
Mama yake Tom, mjane bibi Bhoke Wambura, ilibidi asafiri kutoka nyumbani kwao Tarime kuja kumuuguza mwanaye, naye hakudumu sana akawa amefariki kwa ugonjwa wa shinikizo la damu mwanaye akiwa hana fahamu na kuzikwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwenye makaburi ya Kinondoni kwani haikuwepo hata senti moja ya kutosha kusafirisha maiti kwenda Tarime, Tom akabaki kitandani peke yake, marafiki zake wala hawakuulizia aliendeleaje na wauguzi wala hawakujishughulisha naye sana wakijua alikuwa ni mtu aliyesubiri siku yake, kwa miaka miwili zaidi aliendelea kulala kitandani.
Ilikuwa ni asubuhi siku ya Jumapili, wodi ya Mwaisela ikiwa kimya kabisa, wagonjwa wakiwa wametulia vitandani mwao. Mwanamke mwembamba mrefu, afya yake ikiwa imedhoofika alikuwa akimgeuza Tom kitandani ili amwoshe sababu alikuwa amejisaidia kwenye mashuka, hakuwa muuguzi bali mtu aliyejitokeza kumtunza Tom baada ya kukosa ndugu hata mmoja. Ghafla alishangaa alipomwona Tom amefumbua macho, lilikuwa ni jambo geni kabisa ambalo halikutegemewa kutokea, akashtuka na kumuachia, Tom akazungusha macho yake huku na kule chumbani na baadaye kumkazia sana macho mwanamke huyo.
“Wee Malaya nani amekuambia uje nyumbani kwangu? Hivi wewe mwanamke husikii? Nilishakuambia sikupendi kwanini unanifuatilia? Ondoka hapa, Mayasa akikuta utasema nini? Unataka kunichonganisha na Mayasa wangu? Ondoka upesi vinginevyo nitakupiga!” Tom aliongea akijaribu kunyanyuka kitandani, akashindwa, hapo ndipo akagundua hakuwa na hisia hata kidogo kuanzia shingoni hadi miguuni, hakuelewa ni kitu gani kimetokea.
“Tom! Tulia kwanza, huelewi kilichotokea ndani ya miaka mitano iliyopita, niko hapa kitandani kwako kwa sababu nilichonacho moyoni juu yako ni zaidi ya neno nakupenda, zaidi ya mapenzi; This is Beyond Love!” Aliongea mwanamke huyo akibubujikwa na machozi.
Tom hakuwa na habari juu ya kilichotokea maishani mwake, hakuelewa alikuwa amelala kitandani bila fahamu kwa muda wa miaka mitano, fikra zake zilimtuma kuhisi alikuwa amelala kitandani nyumbani kwake mahali ambako alishampiga marufuku Mariam kufika. Alipozungusha macho yake huku na kule ndani ya chumba alicholala, aliwaona watu wengine wakiwa juu ya vitanda na harufu ilikuwa mbaya tofauti kabisa na nyumbani kwake, akaelewa alipokuwa amelala ni hospitali, mara moja akaanza kuzivuta kumbukumbu zake juu ya kilichotokea mpaka akajikuta yuko mahali pale.
Picha iliyokuwa kichwani mwake kwa haraka, aliyoikumbuka kama kitu kilichotokea mwisho ni yeye akiwa ndani ya gari lake aina ya Vogue, akiwa amefunga vioo vyote huku akipulizwa na kiyoyozi, muziki laini uitwao Hello wa mwanamuziki Lionel Richie ulikuwa ukipigwa taratibu kutoka kwenye spika ambazo hazikuonekana. Shingoni alikuwa amevaa mkufu uliotengenezwa kwa mchanganyiko wa dhahabu, rubi na Almasi ambao thamani yake ilikuwa milioni ishirini na tano.
Si hivyo tu, usoni kulikuwa na miwani ya jua kutoka Kampuni ya DG, thamani yake ikiwa ni milioni moja saa yake ilikuwa ni ya milioni tano, nywele zake zilikuwa zimetengenezwa na kuwekewa dawa iliyozifanya zimeremete na kuwa na mawimbi, alipojiangalia kwenye kioo kilichokuwa juu mbele yake kwenye gari, alitabasamu na kumshukuru Mungu kwa jinsi alivyomuumba akiwa kijana mwenye kuvutia, yeye mwenyewe aliamini hakuwepo mwanamke wa kupindisha kama angeamua kumtokea.
Akijiangalia kupitia kwenye kioo hicho, alifanikiwa kuona gari nyeusi aina ya Rav 4 ikija nyuma yake, hakutilia maanani sana akiamini mwenye gari alikuwa na safari zake na alipojaribu kuangalia vizuri, alimwona msichana mzuri akiwa amekaa nyuma ya usukani.
Tom alizidi kukanyanga mafuta gari hilo likimfuata kiasi cha mita kumi tu nyuma yake mpaka akafika kwenye lango la kuingilia kwenye jumba lake la kifahari eneo la Mikocheni jijini Dar es Salaam, akakanyaga breki na kubonyeza kitufe fulani kando ya mlango ili lango kuu lifungunge aingize gari lake, ghafla bila kutegemea kabla hajakanyaga moto, lango likiwa wazi, alishangaa kuwaona watu wawili waliovaa kininja wakiwa wamesimama kila upande wa gari lake, mmoja akipigapiga dirishani na kumwomba afungue, mshtuko mkubwa ulimpata, akaanza kutetemeka akiwa hajui nini cha kufanya.
Akiwa katika hali hiyo akifahamu kabisa alikuwa ametekwa, mmoja wa watu hao waliotoka kwenye gari lililokuwa nyuma yake, alikipiga kioo cha dirisha kwa kitako cha bunduki, chote kikavunjika na Tom kuwekewa mdomo wa bunduki aina ya SMG shingoni.
“Ndugu yangu, naomba usiniue kama ni gari chukua, niachie roho yangu niko tayari kukuongezea na vito vyote vya thamani nilivyovaa na hata fedha ya mafuta kama utahitaji!”
“Sihitaji fedha yako, nimefuata roho yako!”
“Nani amekutuma?”
“Hilo sio swali!”
Kilichofuata baada ya hapo ni milio miwili ya risasi, moja ikazama kichwani kwa Tom na nyingine shingoni, akaanguka kwenye kiti huku akitokwa damu nyingi. Majambazi wakamchukua na kutupa nje ya gari, wote wawili wakaingia ndani na kuondoka na gari lake kwa kasi ya ajabu, Tom akiachwa amelala ardhini akivuja damu nyingi bila kuwa na fahamu, wakati hayo yakitokea ilikuwa ni saa tatu na nusu ya usiku kwani alikuwa akiwahi nyumbani kuangalia taarifa ya habari ya ITV, saa nne kamili.
Hiyo ndiyo ilikuwa kumbukumbu ya mwisho iliyomwijia kichwani mwake baada ya kujaribu kukumbuka ilikuwaje akawa hospitalini, kichwani mwake alifikiri tukio la kuvamiwa lilitokea jana yake kumbe alikuwa amelala kitandani kwa miaka mitano mfululizo bila kuwa na fahamu akiwa amezungushwa huku na kule duniani kutafuta matibabu, Uingereza, Marekani, Ujerumani, India kote walishindwa kumsaidia ndipo akarejeshwa nyumbani Tanzania, mkewe Mayasa akambwaga hospitali ya Muhimbili na kutokomea akiwa ameuza kila kitu na kumwacha masikini.
“Yuko wapi mke wangu mpenzi Mayasa?”
“Mayasa hakukupenda wewe Tom, alipenda mali zako, zilipokwisha akaamua kukukimbia, mimi niko hapa pembeni mwa kitanda chako kwa sababu niliyokueleza, la kwangu ni zaidi ya penzi!” Aliongea Mariam akilia kwa uchungu, kumbukumbu za mambo yote ambayo Tom alimfanyia zilimwijia, akamwangalia na hasira ikapanda, lakini akakumbuka neno la mwisho alilolisema kabla hajatoka porini kwamba “Nimemsamehe Tom!”
Hali ilikuwa ya utulivu jijini Dar es Salaam, watu wengi walikuwa wakirejea majumbani mwao kutoka kazini, giza lilishaanza kuingia. Katika wakati kama huo watoto wengi maeneo ya Vingunguti, Manzese, Tandika na kwingineko walikoishi watu wenye maisha ya kawaida, walikuwa wakioshwa tayari kwa chakula cha usiku na kwenda kulala, ndio maana vilio vya watoto wengi ambao hawakutaka kuoga vilisikika, labda siku ambayo kwenye nyumba nyingi ulipikwa wali, siku hiyo hakuna mtoto aliyelia, akiogopa kuambiwa ‘mpelekeni akalale’
Nyumbani kwa mzee Maftah Abdallah, aliyekuwa na nyumba kubwa yenye vyumba zaidi ya kumi na tano vilivyojaa wapangaji hali ilikuwa tofauti, watoto walikuwa bado wakicheza na kukimbizana huku na kule uwani, miongoni mwa watoto hao alikuwepo Mariam na Thomas, Mariam akiwa mtoto wa mwenye nyumba na Tom akiwa mtoto wa bwana Chacha, mpangaji aliyefanya kazi ya ulinzi kwenye kiwanda cha Soda cha Pepsi, kilichokuwepo huko huko Vingunguti.
“Tucheze mchezo wa baba na mama, mimi mama wewe baba!” ilikuwa ni sauti ya Mariam akimwambia Tom, ambaye hakukubaliana na mchezo huo, badala yake akawaita watoto wengine wa wapangaji waungane nao kucheza mchezo wa kujificha na kutafutwa, maarufu kwa jina la kombolela, watoto wote wakakubaliana, Mariam akatakiwa kujifunika na viganja vyake machoni na watoto wengine wote wakaenda kujificha, Tom akajificha kwenye nyumba ya kuku.
“Tiari bado?” Mariam aliuliza.
“Bado” watoto wengine ambao walikuwa bado hawajajificha waliitikia.
“Tiari bado?” Mariam akapataza sauti na kuuliza tena mara ya pili,
“Tiari!” Sauti za watoto zilisikika kutoka sehemu mbalimbali walizokuwa wamejificha, akaanza kuwatafuta mmoja baada ya mwingine, ndani ya muda wa nusu saa alishawaona wote lakini akabaki Tom peke yake, Mariam hakukata tamaa akizunguka huku na kule kufunua kila sehemu akimtafuta lakini hakumpata mwisho giza likazidi kuingia, watoto wengine wakaanza kuchukuliwa na wazazi wao kwenda kuoshwa.
“Labda kwenye nyumba ya kuku?” Alijiuliza Mariam ambaye kwa wakati huo alikuwa na umri wa miaka saba, mwanafunzi wa darasa la kwanza shule ya msingi Vingunguti na Tom miaka kumi mwanafunzi wa darasa la pili katika shule hiyo hiyo.
Taratibu akaanza kuisogelea nyumba ya kuku, ndani yake hapakuwa na kuku hata mmoja, wote walishakufa, akapiga magoti chini na kuanza kutambaa akiingia ndani yake, macho yake hayakuamini alipomwona Tom amelala kwenye kona, akataka kupiga kelele kuashiria kwamba amemwona, kabla hajafanya hivyo kiganja cha Tom tayari kilishaufunika mdomo wake kuzuia asiseme chochote.
SOMA HAPA 👉 Chombezotu.blogspot.com
INAENDELEA
Simulizi: Beyond Love (Zaidi Ya Mapenzi) Sehemu Ya Pili (02)
Chombezotu.blogspot.com
“Mimi baba wewe mama, sawa?”
“Sawa!”
“Tulale kama vile baba na mama!”
“Sawa!”
Karibu wapangaji wote wa mzee Maftah walikuwa na chumba kimoja, wakiwa wamegawa katikati kwa pazia ili watoto walale upande wa pili, kwa wenye mtoto mmoja kama ilivyokuwa kwa Chacha na mkewe, hawakuona sababu ya kufanya hivyo, walilala na mtoto wao chumba kimoja wakijidanganya kwamba walikuwa ni watoto wadogo wasioelewa chochote, jambo ambalo halikuwa na ukweli, katika umri wa miaka kumi, Tom aliona kila kitu ambacho wazazi wake walifanya usiku wakiamini yuko usingizini na hicho ndicho alitaka kukifanya na Mariam. Akapanda juu yake.
“Mariaaam!Mariaaaam!Mariaaaam!” ilikuwa ni sauti ya Bi. Mwamtumu Maftah, mke wa baba mwenye nyumba akimtafuta mwanae wa mwisho ili aoge, Mariam hakuitika, aliendelea kubaki kimya Tom akiwa juu ya kifua chake, bila kuelewa jambo alilokuwa akifanya, kwao kilichokuwa kikitokea ni kuwaigiza baba na mama bila kuelewa maana yake.
“Mariaam!” aliendelea kuita lakini sauti ya mtoto wake haikusikika.
Ghafla akipita kando ya kibanda cha kuku alisikia minong’ono ya watoto “baba Khadija, niachie mwenzio watoto hawajalala” moyo wake ukashtuka, akarudi kinyumenyume mpaka kwenye kibanda hicho, akasikia sauti ya mtoto wa kiume “Wewe mama Tom, ritomu rimesharara, sogea huku” hiyo ilikuwa ni sauti ya Tom akimwigiza baba yake, mama yake Mariam hakuyaamini masikio yake baada ya kuhakikisha kabisa kwamba ni binti yake mdogo wa miaka sita na mtoto wa mpangaji wake walikuwa ndani ya kibanda cha kuku wakifanya mambo yasiyolingana na umri wao, akakimbia mbio hadi ndani kumwita mume wake.
“Hebu sikiliza mwenyewe kinachoendelea ndani ya hiki kibanda!” alimwambia mume wake ambaye baada ya kutega sikio, naye pia hakuamini, lilikuwa ni jambo la ajabu mno, hasira zikampanda.
“Hebu kawaite wazazi wa Tom, huyu mtoto wao atatuharibia mwanetu, mtoto ana miaka kumi keshaanza mambo haya? Wallah hatumtaki ndani ya nyumba yetu, lazima wahame!”
Mzee Chacha na mkewe walipoitwa hata wao hawakuamini walichokiona, walishindwa kuelewa ni lini Tom alikuwa amejifunza jambo la hatari kiasi hicho, alikuwa mdogo mno kuelewa mambo ya watu wakubwa, hawakuwa na habari kwamba kila kitu walichokifanya chumbani wakidhani amelala yeye alikiona na ndicho alichokuwa akikifanyia kazi.
“Hizi nyumba zetu za kupanga hizi? Kulala chumba kimoja na watoto ni balaa, inaleta shida sana kwenye malezi!”
“Unaongea kitu gani wewe Chacha, kwa hiyo unataka kutoa kisingizio kwamba nyumba ya kupanga ndio imefanya mwanao atake kuniharibia binti yangu? Usinitanie, jiandaeni kuhama, siwataki tena kwenye nyumba yangu!” mzee Maftah alifoka, Chacha na mkewe wakaweka mikono yao midomoni kwa mshangao, hakuamini kauli waliyoisikia kama kweli ililingana na kosa lililofanywa na watoto.
Maneno hayo hayakuwa utani, mzee Maftah aliandika notisi na kuwakabidhi siku hiyo hiyo akiwataka wahame ndani ya nyumba yake. Hawakuwa na la kufanya zaidi ya kukubali suala likawa ni wapi wangehamia, miezi mitatu baadaye notisi yao ilipokwisha walihamia kwenye nyumba nyingine jirani kabisa na shule ya msingi Vingunguti, mwendo wa dakika tano tu kufika shuleni, Tom akafurahi lakini akiwa na masikitiko mengi moyoni mwake sababu ya kutenganishwa na Mariam, alikuwa amezoea sana kucheza naye.
Mzee Maftah na mkewe walifikiri kuwatenganisha Tom na Mariam ingesaidia, jambo ambalo halikuwa kweli, ukaribu wao uliendelea kama kawaida wakiwa shuleni! Waliongea, walicheza na kufurahi pamoja lakini hawakudiriki tena kufanya mambo yaliyowasababisha wachapwe, Tom aliogopa mno, alama za fimbo bado zilikuwepo mwilini mwake na kila siku aliporejea nyumbani alionywa na wazazi wake kutojishughulisha na mambo hayo tena, akipewa kila aina ya vitisho ili aogope tendo la ndoa, hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Mariam, naye alitishwa kupita kiasi.
Kwa miaka mitano iliyofuata mpaka Tom anamaliza darasa la saba, hawakuwahi kabisa kuongelea suala la mapenzi. Akafaulu kuendelea kidato cha kwanza kwenye shule ya sekondari Ukonga, hapakuwahi kutokea mwanafunzi mwingine aliyefaulu vizuri kiasi hicho, alisifiwa na kila mwalimu, alipewa zawadi mbele ya wazazi na wanafunzi wote na wakatakiwa waige mfano wake! Ilikuwa ni heshima kubwa sana kwa mzee Chacha na mkewe kusimamishwa mbele ya wageni wote waalikwa siku ya kuwapongeza wanafunzi wote waliofaulu.
“Hongera sana Tom!” Mariam alimwambia baada ya sherehe hiyo.
“Ahsante! Inabidi pia wewe uongeze bidii, una uwezo wa kufanya vizuri, jiepushe na mambo yaliyosababisha tukachapwa baada ya kufumwa kwenye nyumba ya kuku, si unakumbuka?”
Badala ya kujibu Mariam alitabasamu na uzuri wote wa sura yake ukaonekana, kimoyomoyo Tom akakiri kwamba Mariam alikuwa msichana mzuri na kuweka ahadi kwamba kama akifanikiwa kufanya vizuri katika masomo yake na kufika Chuo Kikuu hatimaye kupata kazi nzuri angemuoa, hakutaka kuyaweka maneno hayo wazi, alitaka kila kitu kibaki siri mpaka wakati muafaka ufike.
“Nitajitahidi sana kufuata nyayo zako Tom!”
Sababu ya umasikini hata kutimiza mahitaji ya shule, ilikuwa ni kazi ngumu kwa Tom,baba yake alijitahidi kufanya mpaka kazi za kuzibua mitaro akafanikiwa kupata ada peke yake, mpaka zikiwa zimebaki siku nne shule ifunguliwe, Tom alikuwa hajapata sare za shule na godoro. Hakuwa na mahali pa kukimbilia, ikabidi amfuate Mariam na kumwelezea kilichotokea, msichana huyo akamchukua mpaka kwa baba yake na kulia akiomba amsaidie, kwa kumwonea huruma mtoto wake, mzee Maftah alimnunulia Tom mahitaji yote yaliyobaki na kuondoka kwenda shule siku nne baadaye.
“Nakushukuru sana Mariam, bila wewe sijui kama ningekwenda shule, nitaukumbuka sana mchango wako maisha yangu yote!”
“Usijali, nahisi moyoni mwangu kuna upendo wa aina fulani kwako Tom!”
“Kweli?”
“Kabisa”
“Basi tuangalie kitu gani Mungu ataleta mbele ya safari”
Mariam alikuwa amefanya ndoto yake itimie, kwa Tom alionekana ni malaika mkombozi kwani bila yeye asingeweza kuendelea na masomo ya sekondari. Akamshukuru Mungu kwa yote yaliyotokea, nyumbani aliwasimulia wazazi wake jinsi alivyopata msaada, hata wao hawakuwa tayari kuamini kama baba yake Mariam aliyewafukuza kwenye nyumba sababu Tom na Mariam walikutwa ndani ya nyumba ya kuku wakicheza mchezo wa baba na mama ndiye aliyempa fedha mtoto wao kukamilisha mahitaji yote ya shule.
Tom alisindikizwa na wazazi wake hadi Ukonga na kukabidhiwa kwa walimu wake, ulikuwa ni mwanzo mpya wa maisha. Kwa alivyokuwa amevaa, haikuhitaji maelezo yoyote kuelewa alikuwa ni mtoto wa masikini. Alibezwa na kupuuzwa na wanafunzi wenzake wengi wao wakiwa ni watoto wa matajiri jijini Dar es Salaam, hii ilimtia Tom hasira na uchungu lakini hakutaka kulipiza kwa mtu yeyote, nguvu zake zote zikaishia kwenye masomo ingawa alitengwa na wanafunzi wenzake.
Miezi mitatu baadaye walipofanya mitihani ya majaribio, matokeo aliyopata Tom yaliwashangaza walimu mpaka wanafunzi, alishika namba moja, akiwa amepata alama mia moja katika kila somo! Heshima ikaanza kupanda, wanafunzi wakaanza kumsogelea na kumfanya rafiki wakimtaka msaada. Hakuwa na kinyongo, alikuwa tayari kumsaidia kila mwanafunzi aliyemwomba kitu bila masharti yoyote, idadi ya marafiki ikaongezeka na Tom akazoea shule ingawa hakumwondoa Mariam katika akili yake, kila siku alikuwemo, alimuwaza wakati wa kula, kunywa na kulala! Alikuwa ni mtu muhimu sana kwake.
Shule ilipofungwa alirejea nyumbani kwa wazazi wake, baba yake alikuwa bado akiendelea na kazi ile ile ya ulinzi kwenye kiwanda cha Soda cha Pepsi na mama yake alifanya kazi ya kuponda kokoto, hiyo ndiyo kazi ambayo Tom alichagua kufanya ili kupata fedha za matumizi shule ikifunguliwa. Kila siku asubuhi aliondoka nyumbani na mama yake kwenda sehemu ilipokuwa ikijengwa barabara na kuchukua mawe kisha kuyasomba hadi karibu na nyumbani kwao ambako walianza kuyaponda kwa kutumia nyundo, kila siku Tom alifanya kazi hiyo na mama yake bila kuchoka.
“Mama kazi hii mpaka lini?”
“Hatuna jinsi mwanangu!”
“Lakini nitakuja kuwapumzisha wazazi wangu, kwani mmehangaika muda mrefu sana!”
“Jitahidi tu kusoma mwanangu!”
“Nitafanya hivyo mama!”
Alitamani sana kumwona Mariam lakini akaogopa kwenda kwao, kumbukumbu za kusababisha wazazi wake wafukuzwe kwenye nyumba bado ziliendelea kuishi akilini mwake, lakini mwisho alipokumbuka wema wa Mariam na wazazi wake walipompa fedha za mahitaji ya shule, aliamua kuweka hofu pembeni na kumuaga mama yake asubuhi moja na kutembea kwa miguu hadi nyumbani kwao, ilikuwa siku ya Jumapili, ambaye hapakuwa na uwezekano wa Mariam kutokuwepo nyumbani.
“Shikamoo mama!” alimwamkia mama yake.
“Marahabaaaa…nani huyu? Tom?”
“Ndio mama”
“Karibu mwanangu habari za shule?”
“Nzuri tu mama”
“Umeongezeka urefu!”
“Ahsante mama! Hamjambo hapa nyumbani?”
“Hatujambo!”
“Mama nimekuja kuwapeni shukrani zangu kwa wema mlionitendea! Sijui baba yupo?”
“Hapana ametoka asubuhi, usijali sana, tulikuwa tukitimiza wajibu, mbona sisi tulishasahau?”
“Mimi nakumbuka mama, nimemkuta Mariam?”
“Yupo…Mariaam!” alijibu mama huyo na kuanza kuita.
“Bee mama!” sauti ya Mariam ilisikika kutoka ndani.
“Njoo huku nje una mgeni!”
Ukimya ukatokea, baadaye Mariam akatokeza nje, alipomwona Tom furaha ilimjaa, akaruka juu na kushangilia huku akimkimbilia lakini alipomfikia alishindwa kumkumbatia baada ya kuona macho ya mama yake yakimwangalia kama vile alitaka kujifunza kitu! Wakashikana mikono na kusalimiana kwa heshima, kama alivyofanya kwa mama yake, Tom pia akamshukuru Mariam kwa wema aliomtendea na kumtaarifu kwamba alikuwa amefunga shule lakini alikuwa akiendelea vizuri, pia akachukua kadi yake ya matokeo na kumwonyesha.
“Umekuwa wa kwanza?”
“Ndio!”
“Amekuwa wa ngapi?” mama aliuliza.
“Wa kwanza mama, Tom ana akili sana, hongera!”
“Ahsante, wewe unaendeleaje?”
“Vizuri ingawa sikuwa wa kwanza, nilishika nafasi ya kumi!”
“Hongera pia, jitahidi mpaka uende sekondari!”
Waliongea mengi lakini mama hakutaka kuondoka, alikuwepo kusikiliza kila kitu kilichotoka midomoni mwao, Tom alipoaga mama hakumruhusu Mariam kumsindikiza, wakashikana mkono na akaondoka kurudi ndani huku akimshuhudia Tom akitembea kwenda nyumbani kwao, fikra za mapenzi zilikuwa zikijengeka ndani ya mioyo ya watoto hao, hakuna kilichokuwa kimebadilika siku walipofumwa ndani ya nyumba ya kuku, pamoja na kuwatenganisha baada ya wazazi wa Tom kufukuzwa nyumbani kwa baba yake Mariam walipokuwa wamepanga, bado waliendelea kupendana.
Nyumbani Tom alimsimulia mama yake kila kitu wakiponda kokoto, siku hiyo kazi hazikufanyika sawasawa, akili yote ikiwa kwa Mariam. Alimfikiria kila aliponyanyua nyundo juu na alimfikiria kila aliposhusha chini na kuvunja jiwe, ubongo wake ulijaa neno “Mariam!Mariam!Mariam” aliamini kwa upendo aliokuwa nao, huyo ndiye msichana aliyemfaa hata baadaye katika maisha yake, ingawa alikuwa bado ni mtoto mdogo alijikuta akifikiria hivyo akiamini upendo aliokuwa nao Mariam ulikuwa ni wa kweli, mtoto wa tajiri kumpenda masikini halikuwa jambo rahisi kukutana nalo.
Maisha yakaendelea, mara kwa mara Mariam akielekea kwenye masomo ya ziada alipita sehemu ambapo Tom na mama yake waliponda kokoto, alimwonea huruma lakini hakuwa na jinsi ya kumsaidia zaidi ya kuchukua sehemu ya nauli yake na kumwachia ili yeye na mama waitumie kununua chakula au maji. Ulikuwa ni upendo wa ajabu, hata mama yake Tom alikiri kwamba Mariam alikuwa na moyo tofauti kabisa na watoto wengine wa matajiri aliowafahamu.
“Kwa jinsi baba yake alivyo na majumba mengi hapa Dar es Salaam, lazima angekuwa na maringo ya kutisha!”
“Hayuko hivyo mama, ana moyo wa huruma sana Mariam!”
“Basi endeleeni na uhusiano huo huo, msigombane wala usije ukamuudhi!”
“Sawa mama!”
Shule zilipofunguliwa Tom aliagana na Mariam na kurejea shule ambako kazi ilikuwa ni moja tu; kusoma ili kulinda heshima aliyokuwa nayo na pia aliamini hiyo ndiyo njia pekee ya kumfikisha juu na kuendelea kuheshimiwa zaidi na jamii iliyomzunguka hata akiwa mkubwa, hakutaka maisha kama ambayo yeye na wazazi wake waliishi, alipenda sana kubadili historia, awe mtoto wa masikini aliyefanikiwa na kuwatia moyo watoto wengine ambao wangekuwa katika maisha kama ya kwake ili kuonyesha kwamba mafanikio ni ya kila mtu.
Utaratibu uliendelea kuwa ule ule, nafasi ya kwanza ilikuwa ni ya kwake mpaka anamaliza kidato cha kwanza na kuingia cha pili, kila mtu alimpenda, walimu walimfurahia na waliamini kabisa ni yeye ndiye angeweza kuiletea heshima shule yao kwenye mitihani ya kidato cha nne kama angeendelea na kasi hiyo hiyo. Kidato cha pili kilikuwa kizuri sana kwake, hasa kwa kuwa pia Mariam alikuwa amefaulu na kujiunga na shule hiyo hiyo kwa kidato cha kwanza, yeye ndiye akawa mwenyeji wake. Furaha ikawa imeongezeka, wasichana wote walioonekana kuwa karibu naye wakimtaka mapenzi, hakusita kuwatambulisha kwa Mariam ili wajue Paka alikuwa ameingia, Panya wote waondoke.
“Huyu ndiye Mariam uliyekuwa ukimwongelea?” wasichana waliuliza.
“Ndio”
“Ni mzuri!”
“Ahsante, hata mimi najua” Tom alitania.
Urafiki wao ulizidi kukomaa na matatizo ya Tom kiuchumi yakapungua kwani Mariam alimsaidia kwa kila kitu, kila alichotumiwa iwe ni chakula, dawa ya meno ama fedha waligawana na kutumia pamoja. Shukrani zake kwa Mariam alizitoa kwa njia ya kumfundisha masomo aliyoyapitia kidato cha kwanza, yeye pia akaanza kufanya vizuri akashika namba moja kwenye kila mtihani, hii iliwafurahisha sana wazazi wa Mariam kiasi kwamba kila walipokuja shuleni kuwatembelea ilikuwa ni lazima waonane na Tom kumpa shukrani zao.
“Tunakushukuru sana Tom na tunaomba utusamehe kwa yote yaliyotokea ukiwa mtoto mdogo nafikiri wazazi wako huwa wanaliongelea sana suala hili nyumbani!”
“Yalishapita wazazi, ulikuwa utoto tu ule!”
“Basi ni vyema endeleeni hivyo hivyo, kila tutakachomtumia Mariam pia kitakuwa cha kwako!”
“Ahsante mama!”
Hiyo ikawa kama ni ruhusa kwao, mapenzi yakaongezeka ingawa hawakudiriki hata siku moja kubusiana wala kufanya ngono na hakuna kati yao aliyewahi kumwambia mwenzake anampenda kingono! Walikuwa marafiki wa kweli ambao kwao neno “Mapenzi” lilikuwa ni zaidi ya kufanya tendo la ndoa, mwaka wa kwanza ukapita wakiwa pamoja, hatimaye ukaja wa pili, Tom akaingia kidato cha nne na kuendelea kufanya vizuri katika masomo yake kuliko ilivyokuwa kwenye vidato vilivyotangulia, walimu wote walimtegemea yeye kupeperusha bendera ya shule ya sekondari Ukonga Kitaifa, nafasi ya kwanza Tanzania nzima iliaminika kuwa yake.
“Tom!”
“Yeah!”
“I am so proud of your success!” (Najivunia mafanikio yako!)
“Thanks!” (Ahsante)
“And I know you are going to perform well in your final exams!” (Na ninajua utafanya vizuri kwenye mitihani yako ya mwisho!)
“I know! My mind is stronger than any challenge ahead” (Najua, akili yangu ni imara kuliko changamoto yoyote mbele yangu!)
“Today I want to tell something!” (Leo nataka kukuambia kitu)
“What is it girl?” (Nini hicho?)
“NAKUPENDA!”
“Najua unanipenda na mimi nakupenda pia!”
“Sikupendi kama tunavyopendana!”
“Unanipendaje?”
“Vile kivingine!”
“Kivingine aje?”
“Tom!”
“Sijakuelewa!”
Mariam alitumia uwezo wake wote wa kujieleza akijaribu kukitoa kilichokuwemo ndani ya moyo wake ili Tom aweze kuelewa ni kiasi gani alimpenda na alihitaji nini kutoka kwake lakini bado Tom alimkatalia, hakuwa tayari kabisa kujiingiza katika uhusiano zaidi ya uliokuwepo, bado aliikumbuka picha ya tukio la utotoni walipofumwa ndani ya nyumba ya kuku wakiigiza kufanya mapenzi, jambo lililosababisha yeye na wazazi wake wafukuzwe kwenye nyumba ya wazazi wa Mariam kwenda kupanga sehemu nyingine, bado taswira ilikuwemo kichwani na ilimfanya amwogope Mariam, hakuwa tayari kukororofishana tena na wazazi wake waliojitolea kuwa wafadhili wa masomo yake kwa miaka yote aliyokaa shuleni.
PATA VICHEKESHO HAPA👉 KUPITIA SIMU YAKO
INAENDELEA....
Simulizi: Beyond Love (Zaidi Ya Mapenzi) Sehemu Ya Tatu (03)
Chombezotu.blogspot.com
“No!No Mariam, we cant be more than this!” (Hapana! Hapana Mariam, hatuwezi kuwa zaidi ya hapa)
“Think twise darling!” (Fikiria mara mbili mpenzi)
“Even if I think about it a dozen times it won’t change a thing!” (Hata nikifikiria mara kumi na mbili, bado haitabadilisha chochote!)
“I love you Tom, with all my heart, please accept me as your lover!” (Nakupenda Tom, kwa moyo wangu wote, tafadhali nipokee kama mpenzi wako!)
“It is not possible darling, let’s just remain good friends, helping one another to achieve our dreams!” (Haiwezekani mpenzi, tuendelee kuwa marafiki, tukisaidiana kutimiza ndoto zetu!)
“I know, but …!(Najua lakini…)
“That is the truth!” ( Huo ndio ukweli) Tom alisisitiza.
Wote wawili walikuwa bado bikra, mpaka wakati huo Tom akiwa kidato cha nne na Mariam cha tatu, walikuwa bado hawajakutana na mtu yeyote kimwili! Halikuwa jambo rahisi sana kwa mtu kuamini, lakini huo ndio ulikuwa ukweli, Tom alikuwa amedhamiria kuutunza mwili wake kama ilivyokuwa kwa Mariam mpaka watakapomaliza Chuo Kikuu, wote wawili wakiwa wamesahau kwamba miili yao ilikuwa ikikua na mihemko kuongezeka, kilichokuwa kikimtokea Mariam hakikuwa ridhaa yake ni mabadiliko ya mwili yaliyokuwa yakimsukuma, alihitaji sana kufanya tendo la ndoa na mtu pekee wa kufanya naye hakuwa mwingine isipokuwa Tom, alimpenda kwa moyo wake wote.
Kumkatalia msichana mwenye umbile na sura nzuri kama Mariam ilihitaji moyo, haikuwa rahisi sana kwa vijana wengi hasa wa umri kama aliokuwa nao Tom, yeye pia mwili wake ulikuwa ukichemka ni kweli alivutiwa na Mariam kwa kila kitu lakini alijitahidi kadri ya uwezo wake kupambana na hisia zote zilizokuwa zikimpata, Mariam alikuwa mzuri, kuanzia juu hadi chini hapakuwa na mahali pa kumkosoa na kila alipopita mbele ya kundi la wavulana walionekana kupagawa, hakika alikuwa na mvuto wa kutisha, huo ndio ambao Tom alikuwa akipambana nao.
Hakustahimili sana jambo hilo, mwezi mmoja baadaye alijikuta amepunguza msimamo na kuruhusu angalau kuwa wanabusu kwenye kona usiku baada ya kujisomea, hii ilikuwa ni faraja tosha kwa Mariam aliyeamini lazima nia aliyokuwa nayo ingetimia! Kila siku usiku ilikuwa ni lazima wafanye jambo hilo kabla ya kwenda kulala, jambo pekee ambalo Tom hakuwa tayari kulitenda ni ngono.
“Siwezi Mariam, nilishaweka nadhiri ya kutokukutana na mwanamke mpaka niingie Chuo Kikuu!” alimwambia Mariam siku moja wakiwa gizani kabla ya kwenda kulala, alikuwa akishinikiza wakutane kwenye choo cha shule na kufanya tendo hilo.
“Kidogo tu! Wala haitachukua muda, nakupenda Tom tafadhali kubali!”
“Unaweza kupata mimba halafu wazazi wako wakanichukia tena! Huyo ni shetani Mariam lazima upambane naye, ukimruhusu sana hutamaliza masomo yako, ni afadhali umekutana na mimi ninayeweza kukupa ushauri!”
“Nina kondomu, tutaitumia!”
“Umeitoa wapi?”
“Nilipewa na msichana mmoja darasani kwetu!”
“Hata kama una kondomu siwezi kukubali, tendo la ndoa kabla ya ndoa ni dhambi!”
“Tom utabaki kwenye msimamo huo mpaka lini? Mbona wenzetu wanafanya na wanafunzi wengi pia wananifuata mimi nakataa?”
“Naomba uendelee kukataa hivyo hivyo, hiyo ni kwa faida yako!”
Msimamo wa Tom uliendelea kubaki huo huo mpaka mwisho wa muhula ukafika, shule ikafungwa na wote wakarejea nyumbani. Alijisikia mshindi moyoni mwake baada ya majaribu makubwa ya Mariam ambaye tayari alishaanza kuonyesha chuki kwa sababu ya kukataliwa. Wakiwa nyumbani waliendelea kuwasiliana kama kawaida, wakienda kwenye masomo ya ziada pamoja, wazazi wa Mariam walimfurahia na Tom, hawakuwa na wasiwasi naye kwa kitu chochote, wakiamini angemsaidia mtoto wao kutimiza ndoto bila kuelewa kilichokuwa kikiendelea kichwani mwa Mariam.
Usiku wa manane wiki moja kabla shule haijafunguliwa, Tom alizinduliwa usingizini na kelele za mlango ukigongwa, aliposikiliza vizuri ilikuwa ni sauti ya mama yake. Halikuwa jambo la kawaida mama yake kumgongea usiku, ilipotokea kuna shida ni baba aliyekwenda chumbani kwa Tom kumwamsha, hii ilimshtua na kumfanya anyanyuke haraka kwenda kufungua mlango akiwa amevaa bukta tu.
“Vipi mama?”
“Imebidi tu nikuamshe!”
“Kwani kuna nini?”
“Baba yako!”
“Kawaje? Kalewa halafu anakupiga?” Tom aliuliza kwa mshangao, mara kadhaa huko nyuma ilipotokea baba yake akanywa pombe nyingi alimfanyia fujo mama na hata kufikia hatua ya kumpiga jambo ambalo Tom hakulipenda hata kidogo.
“Hapana anaumwa!”
“Anaumwa?”
“Ndio!”
“Nini?”
“Mkojo umekataa kutoka anasema tangu jana mchana, walinzi wenzake wamemrudisha kutoka kazini!”
Tom hakuongea zaidi, wala kuuliza chochote alichokifanya ni kuchomoka chumbani na kupita sebuleni akielekea chumbani kwa wazazi wake, nyumba yao ilikuwa ni ya vyumba viwili na sebule. Halikuwa jambo la kawaida kwake kuingia chumbani kwa wazazi wake lakini siku hiyo alilazimika kufanya hivyo, akamkuta baba yake amelala sakafuni akitupa miguu huku na kule na kulalamika maumivu ya tumbo, mwili wote ulikuwa umelowa jasho, akitua harufu kali ya mkojo! Ingawa alijua kabisa Tom hakuwa na uwezo wa kumsaidia alianza kulia akiomba ampunguzie maumivu, hali ilimchanganya Tom, akamgeukia mama yake aliyekuwa akilia.
“Mama tufanyeje?”
“Twende hospitali!”
“Tutapata wapi daladala saa hizi?”
“Sijui!”
“Tusaidiane kumbeba mpaka stendi, Mungu atajua huko huko!”
“Sawa mwanangu!”
Wakakubaliana, mzee Chacha alikuwa mzito sana kwao lakini walijitahidi kadri ya uwezo wao na kumbeba juu juu wakipita kwenye madimbwi ya maji sababu mvua kubwa ilikuwa imenyesha jijini Dar es Salaam siku hiyo. Njia nzima mzee Chacha alikuwa akilia kama mtoto mdogo, hata hivyo wakafanikiwa kufika stendi na kumlaza chini, tayari ilikuwa saa tisa na nusu za usiku kwa mujibu wa saa ya plastiki ambayo Tom alikuwa amevaa mkononi, kila gari lililopita walijaribu kulisimamisha lakini hakuna lililosimama, wote wawili wakachanganyikiwa.
“Mama!”
“Naam mwanangu”
“Acha nikimbie nyumbani kwa akina Mariam nikamwombe baba yake atusaidie gari!”
“Wazo zuri sana, laiti ungekuwa umesema mwanzo, hivi sasa tungekuwa hospitali!”
“Nilipitiwa!”
Pamoja na giza lote lililokuwepo Vingunguti sababu ya mawingu ya mvua angani, Tom hakuogopa, ni kweli hakuzoea kutembea usiku kwa kuogopa vibaka lakini siku hiyo aliweza. Akakimbia moja kwa moja hadi nyumbani kwao na Mariam na kuanza kugonga kwenye lango kuu la kuingilia lakini hakuna mtu aliyemsikia wala kufungua, akalazimika kuzunguka nyuma ya nyumba na kugonga kwenye dirisha la kwanza alilokutana nalo bila kujua nani aliyelala ndani ya chumba hicho.
“Nani?” ilikuwa ni sauti ya Mariam.
“Mariam?”
“Ndio!”
“Mimi ni Tom!”
“Tom?”
“Ndio!”
“Unafanya nini saa hivi nje?”
“Baba yangu anaumwa!”
“Anaumwa nini?”
“Ameshindwa kukojoa!”
“Mungu wangu! Sasa?”
“Nimekuja kuomba msaada wa gari!”
“Baba amesafiri, tutafanyaje sasa?”
Tom alikuwa gizani akijaribu kutafakari juu ya nini cha kufanya ili kuhakikisha kwamba baba yake anapelekwa hospitali baada ya kuambiwa na Mariam kuwa gari lilikuwepo lakini baba yake ambaye dereva alikuwa amesafiri, hivyo hapakuwa na dereva wa kuifanya kazi hiyo. Akamwomba Mariam atoke nje ili wapate kushauriana kwa sababu akili yake yeye ilikuwa imekoma kufanya kazi.
“Sidhani kama mama atakubali nitoke nje!”
“Sasa?”
‘Tuongelee hapa hapa!”
“Hakuna njia yoyote unayoweza kuitumia kunisaidia?”
“Nakuhurumia sana Tom lakini sidhani kama naweza, mimi najua kuendesha gari lakini sio sana, hata mara moja sijawahi kuendesha gari mbali na hapa nyumbani tena baba akiwa hayupo!”
“Kwa hiyo unaweza kuendesha?”
“Kidogo naweza!”
“Sasa kwanini usijaribu?”
“Naogopa kugongana na magari barabarani!”
“Lakini hakuna magari mengi hivi sasa!”
“Mh! Tom unanishawishi kufanya jambo la hatari sana”
“Mariam take risk for me!” (Mariam thubutu kwa ajili yangu)
“Hebu subiri!” Mariam aliongea akishuka kitandani kisha kunyata hadi sebuleni ambako aligusa juu ya kabati mahali ambako siku zote ufunguo wa gari ulihifadhiwa na kukuta upo, akauchukua na kunyata tena hadi chumbani ambako alimwomba Tom amsubiri nje ya lango.
“Sawa!”
Baada ya kuvaa nguo zake, Mariam alinyata kwa mara nyingine akitumia ustadi wa paka mpaka akaufikia mlango na kuufungua bila kelele yoyote kisha kutembea hadi kwenye lango la kutokea nje, pia akalifungua na kutoka. Tom alikuwa akimsubiri, akamsogelea na wakakumbatiana, Mariam alipomwangalia vizuri aligundua machozi yalikuwa yakimtoka.
“Usilie Tom!”
“Nampenda sana baba yangu!”
“Najua!”
“Naomba unisaidie baba afike hospitali, nakufanyisha kosa lakini sina jinsi, wewe peke yake ndiye msaada ninaoutegemea, tafadhali nisaidie ili baba yangu apone, Mariam unataka niendelee na shule?”
“Ndio!”
“Basi nisaidie ili baba yangu apone, akifa sina uhakika kama naweza kuendelea kusoma!” aliongea Tom akilia, maneno hayo yakauchoma moyo wa Mariam mpaka ndani kama vile mkuki wa moto, naye akalengwalwengwa na machozi..
“Sasa sikiliza!” Mariam alisema.
“Ndio!”
“Nafungua lango kuu, kwa sababu sitaki kuliwasha gari likiwa mahali lilipo, mama atasikia muungurumo, hivyo basi itabidi tulisukume sisi wenyewe kulitoa ndani mpaka pale mbele kwenye mteremko ndipo tuliwashe, huo ndio mtihani tulionao, tukifanikiwa basi mimi niko tayari kuthubutu kuendesha gari kwenda hospitali, si ni Amana Ilala?”
“Ndio!’
“Uko tayari kusukuma gari?”
“Natamani lingekuwa limeshafika nje” Tom aliongea akionyesha utayari wake.
SOMA HAPA VICHEKESHO KUPITIA SIMU YAKO
INAENDELEA
Simulizi: Beyond Love (Zaidi ya Mapenzi) Sehemu Ya Nne (04)
Chombezotu.blogspot.com
Bila woga Mariam akanyata tena na kuingia ndani ambako kwa taratibu sana alizungusha komeo la lango na kufanikiwa kufungua bila kelele ndipo akamwita Tom aingie ndani, wote wawili kwa nguvu zao zote walizokuwa nazo na hata za akiba, walishirikiana na kufanikiwa kusukuma gari hilo dogo aina ya Nissan Datsun hadi nje ambako waliendelea kusukuma mpaka mbele mita kama hamsini hivi, kilichowasaidia ni mteremko, ndipo Mariam akaingia na kuketi kwenye usukani, mara moja akawasha na gari likaitika. Tom alibaki mdomo wazi, hata siku moja hakuwahi kufahamu kwamba msichana huyo alikuwa na uwezo wa kuendesha.
“Nani alikufundisha kuendesha gari Mariam?”
“Ni baba, lakini hajawahi hata siku moja kuniruhusu niendeshe peke yangu!”
“Haya twende basi!”
“Umesema wako sehemu gani?”
“Stendi”
Mariam aliendesha gari kwa ustadi mkubwa, wakipita kwenye barabara zenye madimbwi mpaka wakafanikiwa kufika stendi na kuwakuta wazazi wa Tom wakisubiri, wote wamelowa na mvua, baba akiendelea kulia kwa maumivu makali aliyokuwa nayo yaliyosababishwa na mkojo uliogoma kutoka! Mama yake Tom hakuamini alipoona gari linasimama na mwanae kushuka, macho yake alipoyatupa kwenye usukani alimwona Mariam ameketi, hakutaka hata kuuliza swali lolote, alichokihitaji wakati huo ni kufika hospitali tu.
Baada ya kuegesha gari Mariam alishuka, wote wakasaidiana kumpandisha mgonjwa garini, zoezi lilipokamilika wote wakapanda, gari likawashwa tena na safari kwenda hospitali ya Amana ikaanza. Akiwa nyuma ya usukani Mariam alitetemeka lakini hakutaka kuionyesha hali hiyo, mpaka wakafika Tazara ambako alikata kushoto kuelekea Buguruni ambako alikata kulia kuingia barabara ya Uhuru bila kukutana hata na gari moja barabarani, akanyoosha moja kwa moja hadi hospitali ya Ilala Amana, yeye mwenyewe hakuamini kama alikuwa amewafikisha.
“Nakushukuru Mungu!” alitamka maneno hayo kimoyomoyo alipoegesha gari mbele ya jengo lililoandikwa OPD na wauguzi wakafika wakiwa na machela.
“Vipi?” mmoja wao akauliza.
“Tuna mgonjwa!”
“Anaumwa nini?”
“Ameshindwa kukojoa!”
“Poleni!”
Wauguzi wakapanda ndani ya gari na kwa kusaidiana na Tom pamoja na Mariam walimshusha mgonjwa na kumlaza juu ya machela ambayo ilisukumwa moja kwa moja hadi kwenye chumba cha daktari, akalazwa kitandani na daktari kuanza kumchunguza kwa makini, alishangazwa na jinsi mfuko wa mkojo ulivyokuwa umetuna.
“Mzee hujakojoa tangu saa ngapi?”
“Tangu juzi!”
“Pole sana…masista hebu nileteeni Catheter na vifaa vyote vya Catheterization haraka” Daktari aliagiza.
“Sawa daktari!” Mmoja wao aliitikia na kuondoka mbio aliporejea alikuwa amebeba sinia lenye vifaa pamoja na mpira wa kutolea mkojo, vyote akaviweka kwenye meza iliyokuwa kando ya kitanda, daktari akawaomba ndugu wa mgonjwa watoke nje ili apate kufanya kazi yake.
Tom, Mariam na mama yake wakatoka nje. Alichokifanya daktari ni kuchukua mpira na kuuingiza kwenye uume wa mzee Chacha na kuusukuma moja kwa moja mpaka kwenye mfuko wa mkojo, ilikuwa ni kazi ngumu kidogo kuliko alivyofanya kwa wagonjwa wengine lakini ulipoingia mkojo mwingi ukatoka kwa nguvu na kuanza kujaa kwenye mfuko wa plastiki ambao mpira wa kutolea mkojo ulikuwa umeunganishwa nao. Mzee Chacha akashusha pumzi na maumivu yote yakaisha.
Nje ya chumba cha daktari, Mariam na Tom waliendelea kuongea mama akiwa kimya, fikra zote zikiwa zimetekwa na tatizo la mume wake. Hakuwa na uhakika kama angeweza kupona, ilikuwa ni mara ya kwanza kushuhudia binadamu ameshindwa kukojoa, hakuna kitu alichotamani kama mume wake kupona kwani maisha katika jiji la Dar es Salaam yasingewezekana bila yeye kuwepo, mshahara wake wa ulinzi ulikuwa mdogo lakini uliweza kuitunza familia yao.
“Tom!”
“Naam”
“Acha mimi nirudishe gari la wao kabla hakujakucha, mama yangu huwa ana kawaida ya kuamka saa kumi na mbili kamili, hivi sasa ndio nasikia Adhana inalia, acha nirudi, ili mradi nimeshakufikisha hapa, endeleeni na matibabu nitakuja kukuona asubuhi!”
“Nakushukuru sana Mariam, msaada ulioutoa ni mkubwa sitausahau, nakupenda kuliko unavyofikiria!”
“Nakupenda pia na ndio sababu nayafanya yote haya!”
“Endesha vizuri njiani, naomba Mungu asaidie ufike nyumbani salama!”
“Amina!”
Wote wakasimama na kukumbatiana, walipoachiana ndipo Mariam alimfuata mama yake Tom na kumuaga, yeye pia alitoa shukrani nyingi na kumtaka pia afikishe shukrani hizo kwa wazazi, hakuwa na habari kabisa kwamba gari liliibiwa. Mariam akashukuru na kuingia ndani ya gari, kuwasha na kuondoka kwa mwendo wa kawaida.
Mbele aliingia barabara kuu ya Uhuru na kunyoosha kama alivyokuja mpaka akafika Tazara kwenye mataa, macho alipoyatupa mbele aliona taa za kijani zikiwaka, akawa na uhakika ilikuwa ni zamu yake, kwa haraka aliyokuwa nayo wala hakutaka kuangalia upande mwingine wowote, akakata kona kuelekea uwanja wa ndege, hakujua kama kulikuwa na daladala la kutokea Mbagala likija kwa kasi bila kujali taa alishtuka, aliona mwanga mkali machoni.
“Mamaaaaaaa! Nakufa!” ndio maneno pekee aliyoyasema ukatokea ukimya.
***
“Tumeutoa mkojo sasa hivi anajisikia vizuri, lakini ni lazima tufanye uchunguzi ili kufahamu ni kwanini alishindwa kukojoa, hapa kuna uwezekano kukawa na moja kati ya matatizo mawili, aidha ana Stricture au Benign Prostatic Hypertrophy!” daktari aliongea baada ya kuwaita Tom na mama yake kutoka nje.
“Sijakuelewa daktari” Tom alisema, maneno yaliyokuwa yametolea yalikuwa ni mazito sana kwa elimu yake ya kidato cha nne.
“Inawezekana kuna kovu ambalo limeziba njia ya mkojo, hii inaitwa Stricture au Tezi ya Prosteti imepanuka sababu ya uzee na kuuziba mrija wa kutoa mkojo nje sababu unapita ndani yake!”
“Mungu wangu si ni magonjwa makubwa sana hayo?”
“Hapana, yanaweza kutibika kwa njia ya upasuaji lakini ni lazima tufanye kwanza uchunguzi kupata uhakika! Subiri kuche, ili afanyiwe vipimo vya Ultra-sound ili tuone kama kuna tatizo lolote tumboni, sawa?”
“Sawa daktari!”
“Kwa hivi sasa naandika cheti akalazwe wodi ya wanaume!”
“Ahsante daktari!” mama yake Tom aliitikia.
Kulipokucha hapakuwa na kazi nyingine iliyofanyika hospitali kwa mzee Chacha zaidi ya vipimo, daktari aliandika kwenye faili lake afanyiwe kipimo cha kupiga picha tumboni kilichoitwa kwa kimombo Ultra-sound, saa tatu kamili wauguzi walifika na kumbeba kwenye machela kumpeleka kwenye chumba cha kipimo hicho, mrija wa mkojo ukiwa mahali pake. Kila kitu kikafanyika na akarejeshwa wodini baada ya dakika arobaini na tano, Tom na mama yake walikuwepo kusubiri, mioyo yao ikiwa na hamu kubwa ya kujua tatizo lililokuwa likimsumbua mgonjwa wao.
“Tom!” Dk. Magesa alifika na kumwita nusu saa baadaye, mkononi akiwa ameshikilia faili juu yake likiwa limeandikwa Chacha Mitiro, Tom akaelewa lilikuwa ni faili la baba yake.
“Naam daktari”
“Njoo wewe na mama tuongee!”
Akamgusa begani mama yake alikuwa akisinzia kwenye msingi nje ya wodi na kumwomba anyanyuke wafuatane, wakaingia wodini ambako wauguzi walikuwa bado wakimsaidia mzee Chacha kupanda kitandani. Daktari akaanza kufungua faili lililokuwa mikononi mwake, wakati anamaliza wauguzi nao walishamaliza kumlaza mgonjwa kitandani ndipo daktari akaanza kulielezea vizuri tatizo lililokuwa likimsumbua mzee Chacha.
“Mzee anaumwa, ana uvimbe tumboni!”
“Uvimbe wa nini?” mama yake Tom aliuliza.
“Tezi ya Prostate, kwa ilivyovimba nahisi atakuwa na Saratani, kwani uvimbaji wake sio wa kawaida, nahitaji kumchukua kwenda chumba cha upasuaji leo mchana ili nipate kuchukua kipande cha nyama kwenye tezi hiyo nikipeleke hospitali ya Ocean Road kuhakikisha ninachokiwaza!”
“Sawa tu daktari!”
“Kwa hiyo naomba muwe wavumilivu, kwa hivi sasa atatumia dawa za kuzuia maambukizi lakini pia atakojoa kwa kutumia mpira, tukishapata majibu ndio tutajua sasa ni nini kifanyi…!” daktari hakuimaliza sentensi yake hadi mwisho akashangaa kuona mzee Chacha akikakamaa kitandani kama mtu mwenye degedege kali, lilikuwa jambo la ajabu sana kulishuhudia kwani mara nyingi waliopatwa na tatizo hilo walikuwa ni watoto wadogo.
“Mungu wangu baba kawaje tena?” Tom aliongea akimwangalia daktari.
“Hebu nipeni sindano ya Valium!” daktari aliwaeleza wauguzi huku akimlaza mzee Chacha vizuri kitandani kuhakikisha haumi ulimi wake, muda mfupi baadaye muuguzi alirejea na chupa ya dawa pamoja na bomba la sindano, akamkabidhi daktari ambaye aliivunja na kuinyonya dawa yote kwa kutumia bomba kisha kumchoma mzee Chacha, muda mfupi baadaye akatulia na kulala usingizi.
“Sijui ni kwanini anapatwa degedege? Nahitaji kujua hili suala, sijawahi kuona mtu aliyeshindwa kukojoa akapatwa na hali hii, lazima kuna tatizo jingine hapa!”
“Tusaidie kumchunguza vizuri daktari, huyu ni baba yangu ndiye anayenisomesha, akifa mimi nitakuwa nimekwama moja kwa moja!”
“Unasoma darasa la ngapi Tom?”
“Kidato cha nne!”
“Ulikuwa wa ngapi kwenye mtihani wako?”
“ Wa kwanza!”
“Hongera, unataka kuwa nani ukimaliza masomo yako?”
“Kama wewe”
“Daktari?”
“Ndio!’
“Kazi ya wito hii mwanangu!”
“Nafahamu lakini nataka kusaidia watu, kuna masikini wengi kama mimi!”
“Nakutakia kila la kheri, sasa saa tano kamili watakuja kumchukua wamlete chumba cha upasuaji nichukue hicho kipimo, sawa?”
“Sawa daktari!”
PATA VICHEKESHO KWENYE SIMU YAKO👈 BONYEZA HAPA
INAENDELEA
Simulizi: Beyond Love (Zaidi ya Mapenzi) Sehemu ya Tano (05)
Chombezotu.blogspot.com
Kama ilivyopangwa saa tano kamili machela iliingizwa wodini na mzee Chacha akapandishwa juu yake kisha kupelekwa moja kwa moja hadi chumba cha upasuaji Tom na mama yake wakifuata nyuma na kusubiri nje ya chumba hicho wakiwa na wasiwasi mwingi! Ndani akaingizwa kwenye chumba kimoja kidogo kwa ajili ya kazi hiyo ambako alimkuta Dk. Magesa akimsubiri, kazi ikaanza kufanyika na kukamilika ndani ya kipindi cha nusu saa, haukuwa upasuaji kama ambavyo Tom na mama yake walifikiri bali kifaa fulani kiliingizwa kwa kutumia mashine mpaka kwenye tezi hiyo na kuchukua kipande cha nyama, kikawekwa ndani ya chupa tayari kwa kupelekewa hospitali ya Ocean Road.
Mgonjwa aliporudishwa wodini, mawazo ya Tom yalirejea tena kwa Mariam akaanza kufikiria juu ya wema wote alimtendea, hakujua kabisa angefanya kitu gani ili msichana huyo apate kuzielewa shukrani zake! Hakuwa na jinsi zaidi ya kumpenda, tayari alishaanza kumkubali na kuona kama ingewezekana baadaye katika maisha yao, alikuwa tayari hata kubadili dini yake lakini amuoe Mariam kuwa mke wake wa maisha, mambo aliyomtendea yalikuwa makubwa mno.
“Ananipenda kwa ukweli kabisa!” aliwaza.
Baadaye mama yake aliondoka na kumwacha Tom wodini, kama kawaida aliendelea kumuwaza Mariam akimsubiri kwa hamu, alijua mchana huo ni lazima angefika sababu aliahidi siku hiyo badala ya kwenda kwenye masomo ya ziada angerudi wodini kumwona baba yake Tom. Mpaka saa kumi na moja wakati mama analeta chakula cha jioni, Mariam alikuwa hajaonekana, Tom akahisi labda wazazi wake hawakumruhusu kwani isingekuwa kawaida asifike kabisa kwa upendo aliokuwa nao moyoni mwake.
“Mariam amekuja?”
“Bado”
“Kwanini?”
“Sifahamu mama, lakini atakuja tu!
Walikaa na mama yake mpaka muda wa kuona wagonjwa ukapita bila Mariam kuonekana, mama akaondoka kurudi nyumbani akimwacha Tom mwenye mawazo mengi kichwani mwake, si kwa sababu baba yake alikuwa akiumwa peke yake bali kwa sababu pia Mariam alikuwa hajaonekana, alimpenda mno, alitamani kuwasiliana naye angalau kwa simu lakini hakuwa na namba, matumaini akayahamishia siku iliyofuata ambayo pia Mariam hakuonekana, wasiwasi wake ukazidi kuongezeka.
“Haiwezekani, au kwa sababu kaona baba yangu kaugua? Ndio maana ananitelekeza? Lakini Mariam hawezi kufanya hivyo, ana upendo wa kweli, sijui tu ni kitu gani kimempata!”
Siku tatu baadaye alizobaki wodini akimwangalia baba yake kuanzia sababu mama hakuruhusiwa kulala kwenye wodi ya wanaume, Mariam alikuwa hajaonekana! Badala ya huzuni hisia za chuki zikaanza kumwingia Tom, moyoni akajua alikuwa ametelekezwa kwa sababu baba yake alikuwa mgonjwa. Siku hiyo ndiyo majibu kutoka Ocean Road yalikuja na kuthibitisha kabisa kwamba baba yake Tom alikuwa na Saratani iliyocheleweshwa kupata matibabu na kusambaa karibu kwenye viongo vyote muhimu vya mwili ukiwemo ubongo.
“Ndio maana anapatwa na degedege kumbe ubongo wake umekwishashambuliwa na Saratani!” Dk Magesa aliongea na Tom pamoja na mama yake ofisini.
“Atapona?” Tom aliuliza.
“Kwa kweli ni kazi ngumu kidogo, kwanza itabidi ahamishwe hapa kupelekewa hospitali ya Ocean Road ambako watamwanzishia matibabu ya Saratani, Mungu akisaidia anaweza kupona!”
“Tunashukuru daktari!”
Maelezo hayo baadaye yalitolewa kwa mzee Chacha katika lugha ya kumpa matumaini na wakapakiwa ndani ya gari kwenda hospitali ya Ocean Road, Tom akiwa ameacha maagizo kwa wauguzi kwamba ikitokea Mariam akaonekana na kuulizia basi aelekezwe mahali walikokuwa, wauguzi wakaahidi kumsaidia kufanya hivyo. Safari ya hospitali ya Ocean Road ikaanza, siku zote Tom alipita nje ya hospitali hiyo akielekea feri lakini hakuwahi kuwaza kwamba siku moja angeingia humo akiuguliwa na baba yake, hakuamini kama Saratani ingeweza kuingia ndani ya familia yake, aliuona ugonjwa wa watu wengine.
Matibabu yalianza siku hiyo hiyo kwa njia ya vidonge, mionzi na dawa za sindano ambazo badala ya kuonekana kumsaidia mzee Chacha zilimdhoofisha zaidi, afya yake ikaharibika kabisa na kupoteza uzito mwingi ndani ya muda mfupi! Nywele zote zikanyonyoka kichwani sababu ya ukali wa dawa alizokuwa akipewa.
Kila mara Tom alipomwangalia baba yake alishindwa kuvumilia na kutoka nje ambako alibubujikwa na machozi akitamani angalau Mariam angeonekana na kumpa maneno ya faraja lakini haikuwa hivyo, hatimaye wiki mbili zikakatika hali ya mzee Chacha ikizidi kuwa mbaya, madaktari wakashauri mgonjwa arudishwe nyumbani hasa baada ya kugundua alikuwa ni mtu wa Tarime na mke wake hakuwa tayari azikwe jijini Dar es Salaam kama kingetokea kifo jambo ambalo kila mtu alikuwa akilitarajia.
“Sawa tu daktari nimekubali, tatizo letu kubwa ni nauli, hatuna fedha kabisa!”
“Mimi na wafanyakazi wenzangu tutawachangia fedha kidogo lakini pia ninyi mnaweza mkajitahidi kutafuta kwa ndugu jamaa na marafiki!”
“Tutajitahidi!”
ITAENDELEA
apa apa weka comment apo
Beyond love (zaidi ya mapenzi)
GREEN HACKER
0
Tags
Simulizi za sauti
Chapisha Maoni
TOA MAONI YAKO HAPA